Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akielezea huduma zinazotolewa hospitalini hapo mara baada ya kundi la wasanii wanawake Tanzania kutembelea Hospitali ya Mloganzila hii leo.
Baadhi ya wasanii wanawake wakiwa katika ziara ya kuangalia mafanikio ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Mloganzila.
Muuguzi Odax Myinga wa Muhimbili- Mgonzila (wa pili kushoto) akitoa ufafanuazi kwa wasanii juu ya huduma mbalimbali zinazopatikana katika wodi ya wagonjwa binafsi (private ward).
Naibu Mkurugenzi Dkt. Julieth Magandi, baadhi ya watumishi wa Mloganzila wakiwa katika picha ya pamoja na kundi la wasanii wanawake Tanzania mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo.
………………
Wasanii wanawake Tanzania leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila kwa lengo la kuona mafanikio katika utoaji wa huduma za afya chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema hospitali imekua na mafanikio katika utoaji wa huduma za afya, ikiwemo za kibingwa ambapo hivi karibuni imefanikiwa kupandikiza watoto watatu vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implants) na kwamba hatua hii inaifanya Hospitali ya Mloganzila kuimarika katika utoaji huduma za kibingwa nchini.
‘’Pia Juni mwaka huu kwa mara ya kwanza Mloganzila ilifanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo (cerebral aneurysms) kwa mgonjwa aliyekuwa na tatizo hilo na kuifanya Hospitali hii kuwa ya pili baada ya MOI katika kutoa huduma hiyo’’ amesema Dkt. Magandi.
Kwa mujibu wa Dkt. Magandi Hospitali ya Mloganzila ina jumla ya vitanda 608 na hivyo kuwa hospitali ya tatu kwa ukubwa nchini.
Awali mkuu wa msafara Bi. Mwantumu Mgonja amesema pamoja na mambo mengine ziara hiyo inaangazia miradi mbalimbali iliyotekelezwa na serikali ili kuwaeleza wananchi ambacho serikali imefanya.
“Lengo ni kutembelea miradi ambayo imetekelezwa na serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. John Magufuli, tumepita katika miradi mbalimbali na hii leo tumekuja hapa Hospitali ya Mloganzila ili kujionea wenyewe mafanikio katika utoaji wa huduma za afya na tuwaeleze wananchi juu ya mafanikio haya makubwa’’ amesema Bi.Mgonja .