************************
Na Bashiri Salum, Wizara ya Kilimo
Dodoma.
Serikali imesema inatakutana na wadau wa zao la pamba nchini mapema
mwanzoni mwezi Novemba mwaka huu ili kujadili changamoto zilizopo za
ukosefu wa soko la uhakika na upatikanaji wa viwanda vya kuchakata zao
hilo.
Hayo yamesemwa jana (11.10.2019) na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein
Bashe wakati alipotembelea kiwanda cha Twenty One Century cha mjini
Morogoro kukagua uzalishaji wa bidhaa za pamba.
Akiwa katika kiwanda hicho Naibu Waziri Bashe alibaini changamoto ya
kiwanda kuzalisha bidhaa za pamba tani 24,000 kwa mwaka ambazo
hazilingani na uzalishaji uliopo nchini.
“Kiwanda cha Twenty one Century ambacho ndicho chenye uzalishaji
mkubwa kati ya viwanda vyote vya nguo hapa nchini lakini kinatumia tani
elfu 24 tu za pamba kwa mwaka.” alisema Bashe .
Alibainisha kuwa wakulima mwaka huu wanategemea kuzalisha zaidi ya
tani 700,000 tofauti na mwaka jana zilizalishwa takribani tani 400,000
hivyo kunahitajika viwanda vingi zaidi ili mkulima apate soko la uhakika.
Bashe amesema mkakati wa serikali ni kuona viwanda saba (ginnery) za
Lugulu,Sola, KACU, Mbogwe, Chato, na Manawa zilizopo katika ukanda
unaolima zao la pamba kwa wingi vinafufuliwa haraka.
Mkutano ujao wa wadau utawakutanisha Wawekezaji wa viwanda vya
pamba ,Wachakataji wa pamba (Ginnery), Wizara ya Fedha, Wizara ya
Viwanda na Biashara na Viongozi wa Vyama vya Ushirika ili kujadili
changamoto zinazoikabili sekta ya pamba nchini.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Bashe amepokea malalamiko ya
wawekezaji wa viwanda vya pamba kuhusu uwepo wa kanga na vitenge
vinavyoingizwa nchini vikiwa na ubora hafifu toka nje , hali inayochangia
kushusha bei ya bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.
Naibu Waziri huyo ameahidi kufanyia kazi malalamiko haya ili kulinda soko
la ndani na kuwezesha lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha
uchumi wa viwanda linafanikiwa kwani malighafi ya viwanda inapatikana
kwa wingi toka kwa wakulima.