MKUU wa mkoa wa Morgoro Mhe. Loata Ole Sanare
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa
(hawapo pichani) Oktoba 11 , akiwa katika ziara yake ya kujitamburisha
rasmi kwenye Halmashauri zote Tisa (9) za Mkoa wa Morogoro,ambapo
Halmashauri ya kilosa ni ya pili baada ya hivi karibu kujitambulisha
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole
Sanare(hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kujitamburisha katika
Halmashauri hiyo Oktoba 11.
****************************************
Na, farida saidy – Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amewatoa hofu
wananchi wa Mkoa huo huku akiwahakikishia kuwa yeye ameteuliwa na
Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa kiongozi wa wananchi wote
na kwamba kitakachozingatiwa katika utendaji wake wa kazi ni, Kanuni,
sheria taratibu na miongozo iliyopo.
Mhe Sanare ametoa kauli hiyo Oktoba 11 mwaka huu akiwa katika ziara
ya kujitambulisha rasmi katika Wilaya zote saba (7) zenye Halmashauri
Tisa (9) za Mkoa wa Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ikiwa
ni halmashauri ya pili kwenda kujitambulisha baada ya hivi karibuni
kujitambulisha Katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Akiwa Wilayani Kilosa, Mhe. Sanare amezungumza na makundi
mbalimbali ya Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kundi la Watumishi
wa Halmashauri hiyo, Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali ndani ya
Wilaya ya Kilosa pamoja na Kundi la jamii ya wakulima na wafugaji.
Akiongea na viongozi kutoka Kundi la Jamii ya Wakulima na Wafugaji,
Mhe Sanare amewataka wanamorogoro kuondoa hofu kuhusu utendaji kazi wake na kwamba yeye kutoka jamii ya wafugaji hakumzuii kutekeleza majukumu yake kwa usawa.
“Ni kweli mimi ni mfugaji, lakini ni mfugaji niliyetumwa kuja kufanya
kazi na wafugaji wenzangu kwamba kuna sheria za nchi na taratibu,
tuzifuate. Ni mfugaji niliyetumwa kuja kuwaambia wakulima tuangalie
na haki za wafugaji, na ninyi upande huu tuangalie na haki za upande wa
pili…kwamba Mkuu wa Mkoa aliyekuja si Mkuu wa Mkoa wa Wafugaji
ni Mkuu wa Mkoa wa makundi yote yaliyopo ” alisisitiza Mhe. Sanare.
Kuhusu kukomesha migogoro ya Ardhi amesema migogoro hiyo pamoja
na sababu nyingine kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watendaji wa
Serikali katika ngazi za chini wakiwemo Watendaji wa Vitongoji,
Watendaji wa Vijiji, Kata, Tarafa pamoja na Wenyeviti wa Vijiji.
Kwa sababu hiyo amewataka watendaji hao kujirekebisha, kubadilika na
kuchukua hatua kwa kuwa kuanzia sasa mgogoro wowote wa Ardhi
utakapotokea mtu wa kwanza atakayehojiwa na ikibidi kuchukuliwa
hatua ni Watendaji wote waliotajwa hapo juu.
Katika Hatua nyingine akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilosa Mhe. Sanare amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa
wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo pamoja na Viongozi wa
Halmashauri ya Kilosa kuwarejesha mara moja watumishi wa Idara ya
Uhasibu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha za Umma zaidi ya
Tsh. 700Mil. ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mwisho, Mkuu huyo wa Mkoa kupitia hadhara hiyo aliwahimiza
Wananchi wa Wilaya ya Kilosa kujiandiskisha kwenye daftari la wapiga
kura ili kupata haki zao za msingi za kupiga kura katika uchaguzi ujao
wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu, huku
akiwataka wananchi wakati ukifika wamchague kiongozi mchapa kazi
na mwenye hofu ya Mungu.
Kwa upande wao wawakilishi wa Jamii ya wakulima na wafugaji
walitoa maoni yao kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji
akiwemo Ester Mzindakaya aliyekiri kuwa migogoro hiyo bado ipo
hususan wakulima kwenda kulima maeneo ya wafugaji huku akitoa masikitiko yake kwa Serikali kwa kile alichodai kufutwa kwa Kijiji cha
Mabwegele cha Wilayani Kilosa.
Naye Omary Ally aliomba utaratibu wa uliokuwa unatumika katika
kuendesha Kamati ya Amani ya Wilaya hiyo urejewe kwa kuwa wakati
kamati hiyo inafanyi kazi Migogoro ya Ardhi ilipungua kwa kiasi kubwa
kuliko ilivyo sasa.
Wakati Nangai Nasege kutoka kijiji cha Ihombwe – Mikumi, yeye ni
Mkulima na Mfugaji pia alisema katika eneo lao migogoro hiyo haipo
wanaishi kwa Amani alichoomba ni Serikali kuwezeshe miundombinu
hususan kujengewa malambo kwa ajili ya kupata maji ya kunyweshea
mifugo yao.
Wengi waliopata nafasi ya kuchangia katika mjadala huo walimpongeza
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Adamu Mgoyi kwa kupunguza
migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya Wilaya hiyo, na
wakamuomba Mkuu wa Mkoa amsaidie Mkuu wa Wilaya hiyo hususan
kuwataka watendaji wa ngazi za chini kusimamia kanuni, sheria, taratibu
na sheria ndogo zilizopitishwa na Baraza la Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa ambaye ameaapa kuwashughulikia watendaji
wasiochukua hatua katika kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji
amepokea maoni yaliyotolewa kutoka pande zote mbili za Wakulima na
wafugaji na kwamba wampe muda kupitia michango yao kisha atarudi
Wilayani humo siku za hivi karibuni kutoa majawabu ya yale
waliyochangia.