***********************
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
WANACHAMA sita wa Chama Cha Mapinduzi ,wanaodaiwa kufanya vurugu na kuchana nyaraka baada ya majina yao kutorudi katika mchujo wa wagombea wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za Mitaa, katika kijiji cha Mihuga ,Miono wilayani Bagamoyo wametakiwa kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ,mkoani Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akizungumza katika ziara yake ya kuhamasisha zoezi la uandikishaji kwenye daftari la orodha ya wapiga kura.
Alieleza ,amefikishiwa taarifa ya tukio hilo ambapo watu hao walikimbia na hawajulikani walipo.
“Kama jina lako limechujwa kazi yako sio kufanya vurugu rudi kwa viongozi wako wa kata kaeni na angalieni taratibu ili haki yako ipatikane na sio kufanya vurugu”
“Sitokubali watu kutuharibia uchaguzi wetu ,tuchague viongozi kwa amani na utulivu, na hawa ambao wamefanya kitendo hiki cha uhalifu ,ni lazima wajitokeze kutoa ushirikiano kwa polisi”alieleza Ndikilo.
Ndikilo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Salim Mohammed, Mfumwa Ramadhani, Mwajuma Husen ,Fatuma Kazimili, Kapera Ramadhani na Furaha Zuberi .
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa aliwataka watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika na tukio la kuweka sumu kwenye malisho ya mifugo na kusababisha ng’ombe 15 kufa,huko kijiji cha Miono kujisalimisha polisi ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Ndikilo, amesikitishwa na tukio hilo ambalo linadaiwa kuhusishwa na mmoja wa viongozi wa juu wa kata ya Miono.
Alisema, migogoro ya wakulima na wafugaji imalizwe kwa amani na sio kuwekeana visasi baina ya makundi hayo mawili.