Home Mchanganyiko POSTA DODOMA KUONGEZA WIGO UTOAJI HUDUMA

POSTA DODOMA KUONGEZA WIGO UTOAJI HUDUMA

0

Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania Mkoa wa Dodoma wakikabidhi msaada kwa watoto wa Kituo cha kulea watoto wenye utindio wa ubongo cha Miyuji Cheshire.

Afisa mwandamizi mkuu wa Posta Dodoma, Michael Mwanachuo akiwa na baadhi ya watoto wanaolelewa katika Kituo cha kulea watoto wenye utindio wa ubongo cha Miyuji Cheshire.

wafanyakazi wa shirika la Posta Tanzania Mkoa wa Dodoma wakikabidhi msaada kwa watoto wa Kituo cha kulea watoto wenye utindio wa ubongo cha Miyuji Cheshire.

…………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

SHIRIKA la Posta Tanzania mkoa wa Dodoma limejipanga kuhakikisha linaongeza utoaji wa huduma na usambazaji wa barua, nyaraka, vipeto na vifurushi.

Hayo yameelezwa jijini hapa na Afisa mwandamizi mkuu wa Posta Dodoma, Michael Mwanachuo wakati wa maadhimisho ya miaka 145 ya Umoja wa Posta duniani.

Maadhimisho hayo kwa Mkoa wa Dodoma yamekwenda sambamba na kutoa msaada wa vyakula na vinywaji kwa Kituo cha kulea watoto wenye utindio wa ubongo cha Miyuji Cheshire.

Mwanachuo alisema katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamia Dodoma, Shirika limejizatiti kuhakikisha linasambaza kwa haraka barua, nyaraka vifurushi na vipeto katika jiji la Dodoma sambamba na kwenye mji wa serikali ulioko Mtumba.

“ Ili kuendana na kasi ya awamu ya tano katika kuchangia kukuza uchumi wa kati nchini ifikapo 2025 na uamuzi wa kuhamia Dodoma tumejipanga na sasa tunatekeleza kwa kusambaza kwa haraka na welezi barua, vifurishi na vipeto kwa mtu mmoja mmoja, taasisi na zaidi kwenye mji wa serikali.

Alisema usambazaji wa barua umekuwa rahisi kwa shirika hilo hasa kutokana na eneo kubwa la Mkoa wa Dodoma kuwa na majina ya mitaa au anuani za makazi.

“ Hii kwetu imekuwa ni fursa kubwa hasa ukizingatia kuwa Dodoma ilikuwa ni mikoa mitatu ya mwanza ambayo ilianza utekelezaji wa anuani za makazi, hivyo mji unamitaa yenye majina hata kule ambapo bado hakujaendele tayari kuna mitaa.

“ Kwa kuwa na anuani za makazi imeliwezesha Shirika na wateja wenye anuani sahihi za makazi kufikishiwa barua, vifurushi na vipeto kwa urahisi.”

Akizungumza hatua ya kutoa msaada kwa watoto wenye mahitaji, Mwanachuo alisema wamefikia uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya kutaka kufurahi na watoto hao.

“ Tumeguswa na mahitaji ya watoto hasa wenye mahitaji maalum ndio maana katika kuadhimisha Siku ya Posta Duniani tumeamua tuje kuwaona watoto na kutoa zawadi kama wazazi na jamii ambayo inawajibu wa kushiriki kikamilifu kuwalea watoto hawa.”

Naye Sister Theresia Cosmas wa kituo hicho, walishukuru wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania Mkoa wa Dodoma kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada huo wa vyakula kwani utasaidia kwa kiwango na kwa kuonesha moyo wa upendo kwa watoto hao wenye mahitaji maalum.

“ Kituo chetu kina watoto 29 wenye matatizo ya utindio wa ubonga, tunashukuru kwa msaada huu, kwenu unaonekana mdogo, lakini kwetu na watoto hawa ni jambo kubwa sana la kutupatia chakula, lakini kubwa kuja kufurahi na sisi,” alisema.

Alisema kwa sasa kituo chake kinakabiliwa na tatizo la nishati husani uhaba wa kuni na dawa kwa ajili ya kuwatibia watoto.

“ Siku za nyuma watoto wetu walikuwa wanatibiwa kwa msamaha katika hospitali ya Milembe, lakini sasa hilo limeodolewa hivyo tunauhitaji sana wa dawa kwa ajili ya hawa watoto.”

Sister Theresia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa taasisi nyingine kujitokeza kuwasaidia watoto hao hata kufika katika kituo hicho na kushiriki michezo na watoto wao ili nao wajione ni sehemu ya jamii na wapate upendo unaotakiwa kutoka kwa jamii.