Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigamboni Bibiana Bundala, (kushoto) akitoa vyeti kwa wahitimu ya mafunzo ya kupinga rushwa katika mahafali ya kwanza ya wanachama wa Klabu ya Kupinga Rushwa Mkoa wa Temeke, yaliyofanyika DUCE leo, Juni 6, 2026, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).


Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigamboni Bibiana Bundala akizungumza na wahitimu ya mafunzo ya kupinga rushwa kutoka chuo Cha Diplomasia (FRC), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Sabina Isuja, akizungumza na wahitimu ya mafunzo ya kupinga rushwa kutoka chuo Cha Diplomasia (FRC), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Zaidi ya wahitimu 450 wa Klabu ya Kupinga Rushwa Mkoa wa Temeke kutoka Chuo cha Diplomasia (FRC), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wametunukiwa vyeti na kuaswa kusimamia haki, uadilifu, uwajibikaji na kuwa na ujasiri wa kusema ukweli katika mapambano dhidi ya rushwa.
Akizungumza leo, Juni 6, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke katika mahafali ya kwanza ya wanachama wa Klabu ya Kupinga Rushwa Mkoa wa huo, yaliyofanyika DUCE, Mkuu wa TAKUKURU Kigamboni, Bibiana Bundala, amesema kuwa vita dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mwananchi na si la TAKUKURU.
Bundala amesema klabu za kupinga rushwa zina nafasi kubwa katika kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa uadilifu katika jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Sabina Isuja, amesema elimu ya kupinga rushwa ni nyenzo muhimu katika kujenga jamii yenye maadili na uwajibikaji.
Isuja amewataka wahitimu hao kuwa mfano wa kuigwa kwa kusimamia misingi ya haki na kupinga vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi, masomo na maisha ya kila siku.
“Tunatarajia mtakuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa. Tumia elimu hii kuwaelimisha wengine na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoathiri maendeleo ya jamii yetu,” amesema Isuja.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwahamasisha vijana kujiunga na klabu za kupinga rushwa ili wapate maarifa yatakayowawezesha kutambua, kukataa na kupinga vitendo hivyo tangu wakiwa katika umri mdogo.
Ameeleza kuwa elimu ya kupinga rushwa huwajengea watu ujasiri wa kusimama dhidi ya vitendo vya rushwa bila kuogopa vitisho wala ushawishi wowote. Pia huwasaidia kuelewa athari za rushwa na kufanya maamuzi sahihi yanayolinda rasilimali za umma.
Akizungumza kwa niaba ya Msimamizi wa Wanafunzi, Bw. Salvatory Baregu, amewasihi wahitimu kuwa hazina ya maarifa katika jamii na kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya kupitia matendo yao.
Naye Allahz Baru, akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuelewa kwa kina madhara ya rushwa na umuhimu wa kushiriki katika kujenga jamii inayozingatia uadilifu.
Amesema wahitimu wataendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa popote watakapokuwa, sambamba na kuwajenga vijana kuwa na maadili mema na kulinda maslahi ya wananchi.
“Kwa miaka kadhaa, klabu imeendelea kuwa daraja muhimu la kuwafikia vijana na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii. Pia imekuwa chachu ya kuwahamasisha vijana kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za rushwa,” amesema.
Katika mahafali hayo, TAKUKURU Mkoa wa Temeke imekabidhi vifaa vya michezo, ikiwemo jezi na mipira ya miguu, kwa vyuo vya FRC, TIA na DUCE, hatua hiyo imelenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michezo, huku wakipata elimu ya kupinga rushwa.
