NA DENIS MLOWE IRINGA
WAJASIRIAMALI wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kuzingatia ubunifu katika biashara zao kwa kutambua kwa kina mahitaji ya soko na kuimarisha utambulisho wa bidhaa wanazozalisha ili kuongeza ushindani na kuvutia wateja wengi zaidi.

Rai hiyo imetolewa Mwenyekiti wa UWT wilaya ya  Iringa Mjini, Christina Makwei, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makwei alisema kuwa mafanikio ya biashara yoyote yanatokana na uwezo wa mjasiriamali kuelewa matakwa ya wateja wake pamoja na kuhakikisha bidhaa anazozalisha zinakuwa na alama au nembo zinazotambulika kwa urahisi sokoni.

Alieleza kuwa bidhaa zenye utambulisho maalum hujenga imani kwa wateja na kusaidia kuzitofautisha na bidhaa nyingine zinazopatikana katika soko lenye ushindani mkubwa.

Naye mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo alisema kuwa elimu ya ujasiriamali ina mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kujiajiri na kuongeza kipato chao, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali katika usimamizi wa biashara na matumizi sahihi ya fursa zilizopo.

Baadhi ya washiriki walioshiriki mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewaongezea maarifa ya kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi pamoja na kuwapa mbinu za kuwafikia wateja na kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Mafunzo hayo yalifanyika kuanzia Juni 1 hadi 6, 2026 katika Mkoa wa Iringa na yalibeba kaulimbiu inayosema, “Kila mwananchi anaweza kuwa mjasiriamali; tujifunze, tujiajiri na kujikomboa kiuchumi,” ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kupitia ujasiriamali