Mkuu wa Idara ya Radiolojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Flora Lwakatare akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya tiba radiolojia ambayo inaendelea kutolewa hospitali hapa.
Mtaalam wa tiba radiolojia kutoka Toronto nchini Canada, Dkt. Ash Murray akifafanua jambo kuhusu tiba radiolojia.
Dkt. Lwakatare akiwaonyesha waandishi wa habari vifaa tiba vinavyotumika katika tiba ya radiolojia.
Mtaalam wa tiba radiolojia wa MNH, Iddy Besta akiwaonyesha waandishi wa habari jinsi mgonjwa anavyopatiwa matibabu.
Wataalam wa tiba radiolojia kutoka Muhimbili na nchini Canada wakiwa katika picha ya pamoja.
…………………….
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kutoa huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia (interventional radiology kwa wagonjwa 558 tangu huduma hiyo ianzishwe Novemba 2017.
Tiba hii unahusisha vifaa vya radiolojia kama X-Ray, Fluoroscopy, CT-Scan na Ultrasound ambavyo vinatumika kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Idara ya Radiolojia hospitalini hapa, Dkt. Flora Lwakatare amesema kati ya wagonjwa 558, 274 ni wagonjwa waliokuwa na uvimbe kwenye kinywa na wengine 284 magonjwa mengine.
“Tumeendelea kutoa huduma ya kuweka mipira maalum kwenye mshipa mkubwa wa damu (permanent catheter insertions) ambayo inawanufaisha wagonjwa wa figo ambao wanatumia mfumo wa kusafisha damu (renal dialysis) au wagonjwa wanaopatiwa tiba ya saratani, hii inaondoa usumbufu wa kutumia mishipa midogo ya mikononi ambayo mara nyingi ni ngumu kupatikana hasa kama inatumika mara kwa mara kwa muda mrefu.” amesema Dkt. Lwakatare
Dkt. Lwakatare amesema kwamba hivi sasa wanaendelea kutibu uvimbe kwenye kizazi (uterine fibroids) na hadi sasa wagonjwa wanne wamepatiwa huduma hii kupitia tiba radiolojia kwa kuingiza mpira wenye chembechembe maalum kwenye mishipa ya damu ambazo zinakwenda kuziba mishipa hiyo inayopeleka damu kwenye uvimbe.
Amefafanua jinsi tiba hii inavyofanya kazi kwamba baada ya mishipa kuzibwa uvimbe unakosa damu au chakula chake na hivyo kusinyaa na kufa kabisa.
Amesema tiba radiolojia imesaidia utoaji wa sampuli kutoka kwenye uvimbe sehemu mbalimbali za mwili ambazo si rahisi kufikiwa bila upasuaji mkubwa (surgery), inazibua mirija ya nyongo (percutaneous biliary drainage), kuweka mirija kwenye figo ambayo mirija ya mkojo imeziba (nephrostomy tube placement) na unyonyaji wa uvimbe wenye maji/usaha (percutaneous drainage).
Kuhusu faida za tiba radiolojia, Dkt. Lwakatare amesema kuwa tiba hiyo inafanyika bila kuhusisha upasuaji mkubwa ambao una vihatarishi vingi, pia inaepusha mgonjwa kukaa hospitali kwa muda mrefu kwani wanaofanyiwa tiba radiolojia mara nyingi huweza kurudi nyumbani siku hiyo hiyo.
Pia, kupitia ushirikiano wa MNH na Chuo Kikuu cha Yale na vyuo shiriki Emory na Darmouth vya nchini Marekani ilianzisha programu maalum ya mafunzo ya tiba Radiolojia.
Ambapo wakufunzi mbalimbali wamekuwa wanakuja kwa awamu kuanzia Octoba mwaka 2018,ili kujengewa uwezo kwa watalaam wa ndani .
Katika awamu hii ya kumi na moja timu ya tiba radiolojia imetoa mafunzo kwa wataalamu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ili kuwawezesha kuweka mipira maalamu kwenye mishipa kama ilivyoelezewa kwa lengo likiwa kuwawezesha kuwapatia wagonjwa wa saratani unafuu.