Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano mkuu wa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) Mkoani Manyara uliofanyika mjini Babati, ukiwa na kauli mbiu ya mtetezi wa mkulima ni mkulima mwenyewe.
………………
MTANDAO wa Wakulima Tanzania Mkoani Manyara, wameiomba serikali kupitia wizara ya kilimo kusitisha mpango wa matumizi ya mbegu zilizobadilishwa vinasaba (GMO) ili kuwaepusha kuwa tegemezi wa mbegu kutoka nje kwani teknolojia inayotumika kubadilisha vinasaba vya mbegu bado haipo nchini.
Wakulima hao waliyasema hayo mjini Babati kwenye mkutano mkuu wa mtandao wa wakulima Tanzania (Mviwata) wenye kauli mbiu ya mtetezi wa mkulima ni mkulima mwenyewe.
Mmoja kati ya wakulima hao Lohay Langai alisema mbegu hizo zilizobadilishwa vinasaba (GMO) huwenda zisiwe na tija kulingana na mazingira na hali ya hewa ya maeneo mengi ya hapa nchini.
Langai alisema hali hiyo itasababisha wakulima kuwa tegemezi wa mbegu kutoka nje na hata kuchelewa kupatikana lakini huwenda pia ikaporomosha uchumi wa wakulima.
Mwenyekiti wa Mviwata mkoani Manyara, Mohammed Hussein alisema anadhani serikali italeta mbegu hizo za wakulima wakijua kuwa wanakuja kuboresha kilimo kumbe watakuja kuwafanya wakulima wawe tegemezi.
Hussein alisema haoni sababu ya serikali kuingiza mbegu hizo za GMO na badala yake ingeweza kuboresha mbegu za asili zilizopo kwa sasa na zingeweza kuleta tija lakini siyo kuleta mbegu zilizobadilishwa vinasaba.
“Hizi mbegu zilizobadilishwa vinasaba wanafikiri ndiyo wanakuja kumkomboa mkulima kumbe wanakuja kuwaandaa wakulima kuwa tegemezi wa mbegu kutoka nje ambazo wanaweza wasizipate pia kwa wakati,” alisema Hussein.
Mkulima mwingine Emanuel Nuas alisema wakulima hawazihitaji mbegu hizo kabisa bora zilizopo ziboreshwe na kuwapa wakulima elimu ya masuala ya hewa hapo ndiyo inaweza kusaidia lakini siyo mbegu hizo za GMO.
Mratibu wa Mviwata mkoani Manyara, Martin Pius alisema katika kuendelea kupeana elimu ya masuala ya kilimo wakulima waliopo kwenye mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania Mviwata wanakutanika mjini Babati na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mashirikiano ya ushirika na vyama vya wakulima.
Pius aliwaasa viongozi wa serikali kuwekeza zaidi katika kuimarisha ushirika nchini kwa kuwaajiri wataalam wengi na wenye uelewa wa masuala ya kilimo ili kuweza kutembelea na kutoa elimu hususani ya kimasoko kwa wakulima.
Mgeni rasmi wa siku hiyo, mkuu wa wilaya ya Hanang’ Joseph Mkirikiti alilaumu baadhi ya mashirika na taasisi mbalimbali za kifedha ambazo zimekuwa zikieleza kuhudumia wakulima lakini kiuhalisia hawafiki kwa wakulima hao.
“Ninachotaka kusema ni kuwa kumekuwepo na baadhi ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayozungumza na wakulima lakini hawafiki kwa wakulima kutoa elimu ya namna ya kupata mikopo na pembejeo,” alisema Mkirikiti.
Aliwaasa wakulima wa Mviwata mkoani Manyara kuweka malengo ya kukua na kutokuendelea kujiita wakulima wadogo kila wakati.
“Ninawaomba na nyie wakulima wa Mviwata Manyara msiwe mnajiita wakulima wadogo kila mwaka fikirieni sasa kukuwa, mtakuwa wadogo mpaka lini?” alihoji Mkirikiti.