*************************
NA Mwandishi Wetu, Korogwe
JUMLA ya watu sita wakiwemo watoto wanne na watu wazima wawili wamefariki dunia katika vijiji vya Bungu na Dindila wilayani Korogwe mkoani Tanga kutokana kuangukiwa na nyumba kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia saa 2 usiku wa Oktoba 8 hadi majira ya saa 9 alasiri Oktoba 9.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga SACP Edward Bukombe alisema kuwa mvua hiyo iliyonyesha katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe katika milima ya Usambara ilisababisha barabara kuu ya Arusha -Segera -Dar eneo la Msambiazi Korogwe mjini kutopitika na kufungwa kwa muda kwa tahadhari za kiusalama.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Kissa Gwakisa alithibitisha kwa barabara hiyo kufungwa kwa muda na hadi kwa muda wa saa mbili na baadae kuendelea na safari zake kati ya Tanga, Dar es salam, Lushoto, Moshi, Arusha na Nairobi kupitia Namanga mkoani Arusha yaliruhisiwa.
Akizungumzia vifo vya watu sita, Kamanda Bukombe amesema kuwa watu hao ambao majina yao bado hayajulikana ni katika kijiji cha Dindira mwanamke mmoja na watoto wake wawili waliangukiwa na nyumba usiku mkubwa wakati katika kijiji cha Bungu msichana mmoja anayejulikana kwa jina la Asha Yahaya Ambanyonge alikuwa kalala na wadogo zake wawili ambapo nao wameangukiwa na nyumba na kufariki papo hapo.
Mkazi wa Kijiji cha Mgila kata ya Kwashemshi tarafa ya Bungu Korogwe Vijijini Jabir Hamisi Titu (66) alisema kuwa mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya saa mbili usiku Oktoba 8 hadi majira ya saa 9 alasiri mbali na maafa pia imeharibu miundombinu ya barabara ya Kwashemshi-Mgila yenye urefu wa kilometa 5,imesomba mazao, imesomba matanuri ya matofali ya kuchoma na kuangusha mawe kutoka milimani.
Ameongeza kuwa katika kijiji cha Vingo kata ya Kerenge Mremwa kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja amesombwa na maji na hajulikani alipo alikuwa akijaribu kuangalia bustani yake iliyokuwa bondeni.
“Hii mvua imeleta maafa, imeharibu miundombinu,mazao yamesombwa na maji hakupitiki ” alisema.
Wilayani Muheza katika barabara ya Amani -Muheza kata ya Mbaramo eneo la Msangazi mawasiliano ya barabara yalifungwa kwa muda kutokana na mafuriko yaliyoziba njia.
eneo hilo ni sumbufu kwa muda mrefu kutokana na mkondo wa maji uanoanzia vijiji vya Kibanda, Semngano na Kerenge unaokatisha barabara kuu ya Tanga -Segera ambapo mwaka 1997 palitokea mafuriko yaliyosomba basi la Kampuni ya No Challenge na kusababisha vifo vingi.