Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa hotuba na kuomba Ushirikiano na Viongozi wenzake pamoja na Wananchi wa Mkoa huo katika Mkutano wa kukaribishwa huko Ofisi za Wilaya ya Kusini Unguja, wa kwanza (kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrissa Kitwana, na wa kwanza (kulia) Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Kusini Juma Mussa. .
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrissa Kitwana akisoma muhtasar wa Taarifa ya Wilaya ya Kusini katika Mkutano wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud huko Ofisi za Wilaya ya Kusini Unguja.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kusini Unguja Abdul-azizi Hamadi Ibrahim akitoa maelezo kuhusu Chama Cha Mapinduzi katika Mkutano wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud huko Ofisi za Wilaya ya Kusini Unguja.
Baadhi ya Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na Watendaji wa Mkoa wa Kusini Unguja wakifatilia Mkutano wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud huko Ofisi za Wilaya ya Kusini Unguja.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
………………….
Na Mwashungi Tahir ,Maelezo
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amewahakikishia wananchi wa Mkoa huo kuwa atashirikiana na viongozi wenziwe wa Mkoa huo kutatua changamoto zilizopo.
Amezungumza hayo na watendaji pamoja na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) huko Makunduchi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja wakati wa kukaribishwa na kupewa taarifa za utekelezaji wa kazi katika Wilaya huo.
Amesema atakuwa na utaratibu wa kukaa pamoja na wananchi ili kusikiliza changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
“Nitaweka siku maalum ya kukaa na wananchi wazielezee changamoto zilizopo ndani ya Mkoa huu ili kuzitatua na kuhakikisha tunazifanyia ufumbuzi”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Miongoni mwa changamoto zilizokuweko katika Mkoa huo ni sekta ya Afya, udhalilishaji, mmong’onyoko wa maadili, uingiaji wa wageni kiholela bila ya kufuata sheria za nchi.
Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko kwa ajili ya kuhudumia Wananchi na kufahamu kero zao kwa kila sekta na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuona wanaishi kwa amani na utulivu.
Pia amewaomba vijana wawe watulivu kwani wanaandaliwa mazingira mazuri ya kujipatia maisha kwa kuzitumia fursa zilizopo.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrissa Kitwana Mustafa akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Wilaya hiyo amesema hali ya usalama katika Wilaya hiyo iko vizuri na wananchi wanaendelea kufanya kazi zao kwa amani.
Sambamba na hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Kassim Mtoro Abuu akiwasilisha Muhtasari amesema wamepata mafanikio ya kinga ya chanjo kwa watoto ikiwemo pepo punda na kifaduro.
Aidha wameahidi watakuwa nae karibu Mkuu wa Mkoa kwa kumpa mashirikiano ili aweze kufikisha huduma kwa jamii na kuleta maendeleo katika mkoa huo.