Kaimu mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo
Oktoba 8, 2019 wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba 2019 ambao umeshuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano na Kaimu mkurugenzi wa
Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja leo Oktoba 8, 2019 wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2019 ambao umeshuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.
(Picha zote na MAELEZO)
****************************
Na Mwandishi Wetu
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi septemba, 2019 umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
Hayo yamesemwa na Kaimu mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja wakati akitangaza mfumuko wa bei leo Jijini Dodoma.
“Kushuka kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019 ikilinganishwa na bei za kipindi cha Septemba,2018”. Alisisitiza Bi. Minja.
Akifafanua amesema kuwa baadhi ya bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Septemba ni mafuta ya taa asilimia 1.0, Petroli asilimia 3.3 ,majiko ya gesi asilimia 1.5, dawa za kuulia wadudu nyumbani asilimia 2.2 na mafuta ya nywele asilimia 1.3.
Aliongeza kuwa mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
Akizungumzia nchi za Afrika Mashariki Bi. Minja amesema kuwa mfumuko wa Bei nchini Kenya kwa mwezi Septemba umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka 5.00 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
Kwa upande wa nchi ya Uganda, mfumuko wa Bei kwa mwaka unaoishia mwezi
Septemba 2019 umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.