Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo. Kulia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Balozi Mstaafu John Haule.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katikaukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo.
Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi. Dalahile Malele akiwasilisha malalamiko yake kuhusu kutojibiwa kwa maombi yake ya uhamisho wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa Halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitia saini kitabu cha wageni kabla ya kikao chake na watumishi wa Halmashari ya Wilaya ya Itilima kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
……………………………….
Na Happiness Shayo, Itilima
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, kuacha mara moja tabia ya kuomba uhamisho pasipokuwa na sababu za msingi na badala yake watumie ujuzi walionao ili kuleta maendeleo katika eneo hilo.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa wito huo wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“Ninyi ni wataalamu na mna ujuzi mbalimbali, hivyo wananchi wa Itilima wanahitaji huduma yenu na kuongeza kuwa, kama mnaona Itilima hakuna maslahi kwenu, inawapasa kutumia ujuzi wenu kuhakikisha mnaongeza mapato ili muweze kunufaika na ongezeko hilo” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa amewatahadharisha Maafisa Utumishi kuhakikisha wanajiridhisha na sababu za watumishi kuomba uhamisho na kuhakikisha kuna mbadala wa mtumishi atakayepewa uhamisho, lengo likiwa ni kutoathiri utoaji huduma kwa wananchi.
“Maafisa Utumishi mnatakiwa mjiridhishe na sababu zinazotolewa na watumishi wanaoomba uhamisho kama ni za msingi na iwapo wametengewa bajeti katika mwaka husika”, Dkt. Mwanjelwa amesema.
Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi hao kutulia katika vituo vyao vya kazi ili waweze kuwahudumia wananchi kwani Serikali iliwaajiri kwa sababu hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi. Elizabeth Gumbo amekiri kuwa, wilaya hiyo ina changamoto kubwa ya watumishi kuomba uhamisho hivyo amewataka kutafakari upya ili waendelee kuwatumikia wananchi wa Itilima.
Aidha, Bi. Gumbo ameahidi kuhakikisha watumishi wa wilaya yake wanafanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Simiyu kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji na watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za watumishi hao na kutatua changamoto zinazowakabili.