********************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Paul Makonda ameelekeza Watumishi wa TAMISEMI wanaohusika na Miradi ya ujenzi wa Mifereji na Mito kupitia DMDP kuhakikisha kabla ya October 10 mwaka huu miradi yote ya Ujenzi wa Mifereji Wilaya ya Ilala iwe imeanza na endepo watakaidi atahitisha maandamano ya wakazi wa Kata 5 kwenda Wizara ya TAMISEMI.
RC Makonda ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea Mfereji wa Kisiwani kata ya Buguruni ambao tangu mwezi May mwaka huu aliagiza ufanyiwe maboresho kutokana na mfereji huo kuwa chanzo cha mafuriko kwenye makazi ya watu lakini ameshangazwa kuona hadi leo anafika site anakuta hakuna chochote kilichofanyika licha ya mkataba kusainiwa tokea mwezi wa Saba mwaka huu.
Jambo hilo lilimlazimu RC Makonda kumpigia simu Mratibu wa Miradi ya DMDP Bwana Emmanuel Ndyamkana ambae alijitetea kuwa miradi hiyo inakwama kutokana na wizara ya fedha kuchelewa kutoa fedha jambo ambalo RC Makonda amesema ni uzembe.
Aidha RC Makonda ameitaja baadhi ya Mifereji na Mito inayotakiwa kufanyiwa maboresho ni pamoja Mfereji wa Tabata kanisa la Roman catholic, mfereji wa Kiwalani na baadhi ya Mito yenye urefu wa Km 19 ambayo ujenzi wake utagharimu takribani Shilingi Bilioni 32.
Pamoja na hayo RC Makonda ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Machinjio mpya ya Vingunguti na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambapo amewataka NHC kuhakikisha ujezni unakamilika kwa muda uliopangwa.