Mtendaji Mkuu wa wakala ya Serikali Dkt.Bakari Bakari,akiongea katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) kuhusu jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao.
Ukurasa wa 152
Realistic device mockup white color smartphone
Ukurasa wa kuingilia ( log in page) wa mfumo Shirikishi wa kusimamia Rasimali za Taasisi
Ukurasa wa ndani wa mfumo Shirikishi wa Kusimamia Rasimali za Taasisi ukionyesha Moduli zote.
………………….
Uvumbuzi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) umeleta fursa za maendeleo kwa mtu binafsi au kwa taasisi husika na faida nyingi zisizomithilika katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na maisha kwa ujumla TEHAMA imekuwa ni njia mbadala ya kuhudumia wananchi na inapotumiwa na taasisi za umma katika utekelezaji wa shughuli zake na katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kwa gharama nafuu ndiyo hujulika kama serikali mtandao.
Hivyo, Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha inapata faida zitokanazo na matumizi ya TEHAMA kwa ufanisi, iliamua kuundaa taasisi mpya ambayo ilipewa majukumu ya kuratibu na kusimamia matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma ili ziweze kunufaika ipasavyo katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hivyo, kwa kuzingatia hili Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mh. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb), anasema Serikali ilianzisha Wakala ya Serikali Mtandao iliundwa kwa mujibu wa sheria Na. 30, Sura ya 245 ya mwaka 1997 chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikuwa na jukumu la kusimamia serikali mtandao na kuratibu maendeleo ya TEHAMA ndani ya Serikali na taasisi zake, baada ya kupitia matokeo ya tathmini ya hali halisi ya matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za serikali ambapo taasisi nyingi zilionyesha kujitengenezea mifumo na raslimali nyingine za TEHAMA bila kujali uwepo wa jitihata hizo katika taasisi nyingine. Hali hiyo ilichochea kuwa na urudufu wa jitihata za TEHAMA zinazofanana na zisizowasiliana wala kubadilishana taarifa.
Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla ya Serikali kujikita katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma kwa umma, Mhe. Waziri anaelezea kuwa, Serikali mtandao ni nyenzo inayotumika katika kubadili na kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi. “Kazi hii sio rahisi kuifanikisha, inahitaji rasilimali za kutosha, utashi wa kisiasa, watumishi waliobadilika kimtazamo na kimatendo ili kuhakikisha serikali mtandao inatumika ipasavyo ndani ya Serikali na taasisi zake (G2G), kati ya Serikali na sekta ya biashara (G2B) na kati ya Serikali na wananchi (G2C). Ili kuyafikia yote haya, tunahitaji kubadili mifumo ya utendaji katika Serikali kwa ujumla”.
Naye Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Bw. Priscus anasema kuwa mwananchi anapata manufaa mengi kutokana na matumizi ya TEHAMA kwa kuwa anarahisishiwa upataji wa huduma mbalimbali hapo alipo bila kutembea umbali mrefu na kwa gharama nafuu. Kwa upande wa taasisi za umma, TEHAMA inarahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Akizungumzia mafanikio ya serikali mtandao yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Wakala ya Serikali Mtandao mwaka 2012 hadi sasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala, Dkt. Jabiri Bakari anaeleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa serikali mtandao, husan katika maeneo ya sera, sheria na miongozo, usimamizi, utengenezaji wa mifumo tumizi na ya kimkakati ya TEHAMA, na ujenzi wa miundombinu ya pamoja ya TEHAMA.
Dkt. Bakari anafafanua kuwa, katika hatua za utekelezaji wa majukumu yake, Wakala ilianza na utayarishaji wa mpango mkakati wa miaka mitano ya kwanza (2012/2013 – 2016/2017), ambao ulihuishwa na kutoa mpango mkakati wa pili wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Anaendelea kufafanua kuwa jitihada za awali za kutekeleza malengo haya zilikuwa katika kushiriki katika matayarisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa serikali mtandao kama vile sheria ya miamala ya mwaka 2015, muswada wa sheria ya uhalifu wa mtandao wa mwaka 2015 na kuandaa sheria ya serikali mtandao ambapo muswada wake uliwasilishwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2019.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Serikali Mtandao, Bw. Michael Moshiro, anaeleza kuwa Mafanikio katika utekelezaji wa serikali mtandao yanapatikana kwa kuwa na usimamizi imara. Katika kutekeleza hili Wakala imetayarisha Miongozo, Viwango na Taratibu mbalimbali zinazotumiwa na taasisi za umma katika kubuni, kujenga na kusimamia jitihada mbalimbali za TEHAMA ili kuhakikisha inakidhi mahitaji halisi na kupunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA.
Aidha anaeleza kuwa Viwango, Miongozo na Taratibu hizi zinazopatikana katika Tovuti ya Wakala sehemu ya Miongozo na Viwango https://www.ega.go.tz//standards zinasaidia kuondoa urudufu wa mifumo na kuwezesha mifumo kuwasiliana, kubadilishana taarifa pamoja, kulinda usalama wa taarifa, kuhuisha mifumo kulingana na mahitaji mapya kwa urahisi na kuongeza uwazi na udhibiti wa mifumo hasa inayojihusisha na ukusanyaji na usimamizi wa Fedha kwa ile mifumo iliyotengenezwa au kufanyiwa mapitio na Wakala.
Naye Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka RITA Bi. Robby Otaigo anasema Miongozo na Viwango vinavyotolewa na Serikali Mtandao vikifuatwa vyema vinaleta tija ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Aidha, Wakala inatekeleza mkakati wa kuhakikisha inakuwa na watalaamu wabobezi wa ndani ambao inawatumia katika maeneo yote ya utekelezaji wa serikali mtandao katika kusanifu, kutengeneza, kusimamia na kuendesha mifumo na miundombinu shirikishi ya TEHAMA, kusimamia usalama wa mifumo, miundombinu na taarifa zilizomo na katika usimamizi wa utoaji wa huduma za serikali mtandao kwa taasisi za umma na kusimamia shughuli za ubunifu na utafiti wa jitihada za serikali mtandao kupitia kituo cha utafiti na ubunifu. Anaeleza Dkt. Bakari.
Dkt Bakari anafafanua zaidi kuwa kwa kutumia wataamu wabobezi wa ndani, Wakala ilifanikiwa kusanifu, kutengeneza au kusimamia utengenezaji na uendeshaji wa mifumo tumizi na shirikishi
mbalimbali ikiwemo ile ya kimkakati kwa ajili yake yenyewe au kwa ajili ya matumizi ya taasisi mbalimbali za umma kama vile Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS) unaotumiwa na taasisi za umma 401 zikiwemo ofisi za Ubalozi nje ya nchi kwa ajili ya kubadilishana taarifa Serikalini na Mfumo wa ofisi mtandao (GeOS) unaotumiwa na taasisi 60 unarahisisha shughuli za utawala za kila siku hususani mzunguko wa majalada na nyaraka ndani na miongoni mwa taasisi za umma.
Mifumo mingine ni pamoja na Mfumo wa Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG) uliotengenezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango unaotumika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya taasisi za umma. Mfumo huu unatumiwa na taasisi za umma 524, watoa huduma za malipo 19 ambao ni Benki Kubwa 12 (NMB, STANBIC, NBC, CRDB, EXIM, TIB, BOT, ECOBANK, PBZ, DCB, DTB, na TPB), Mifumo ya Fedha ya Simu za Mkononi 5 (Tpesa, TigoPesa, HaloPesa, Mpesa, EzyPesa na Airtel Money), mpaka sasa.
Anaendelea kufafanua mifumo mingine kuwa ni pamoja na Mfumo wa kuomba vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa watumishi wa umma (https://safari.gov.go.tz) unaotumiwa na taasisi 436 , Mfumo wa Ajira (http://portal.ajira.go.tz) unaotumika katika kuratibu zoezi zima la kupokea na kuchakata maombi ya ajira katika taasisi zote za umma, Tovuti Kuu ya Taifa (www.tanzania.go.tz) iliyohuishwa kutokana na tovuti ya Serikali inayosimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambayo ni dirisha moja la kutolea huduma kwa wananchi na Mfumo wa Huduma kwa Wateja unaotumiwa na taasisi 392 ambao hadi sasa umepokea na kushughulikia maombi ya misaada 6230 ya wateja.
Mfumo mwingine ni Mfumo Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS) ambao ulitengenezwa kwa matumizi ya Wakala pia unaweza kutumiwa na taasisi nyingine za umma baada ya marekebisho kidogo. Kwa sasa unatumiwa nataasisi (4) ambazo ni Wakala yenyewe, Bodi ya Taifa wa Wahasibu na Wakaguzi, Tume ya Ushirika na Tume ya Sayansi na teknolojia.
Akiuelezea kwa kina mfumo wa ERMS, Dkt Bakari anasema, mfumo huu una moduli kumi na nane (18) zinazotegemeana na zinazounganisha shughuli mbalimbali za utendaji kazi ili kuwezesha kubadilishana taarifa miongoni mwa idara/vitengo na kusimamia raslimali kama vile watu, fedha na vitendea kazi, ankra za bidhaa na huduma, mapato na matumizi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli kulingana na mipango na bajeti, usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya watumishi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi, utekelezaji wa shughuli za ununuzi na utayarishaji wa taarifa mbalimbali za utendaji.
Aidha, Dkt. Bakari anafafanua zaidi kuwa, mfumo huu una “dashboard” ambayo inawawezesha Maafisa Masuuli na watumiaji wengine wa mfumo kupata taarifa mbalimbali kulingana na mahitaji yao. Taarifa hizo zinaweza kuwa za fedha, vifungu vya bajeti na bakaa ya fedha, hali ya matumizi ya fedha, taarifa zinazosaidia katika upimaji wa utendaji wa watumishi, na hivyo kusaidia katika utoaji wa maamuzi sahihi.
Kutilia mkazo maelezo yake, Dkt. Bakari anasema ERMS pia inaweza kuunganishwa na kubadilishana taarifa na mifumo mingine Mikuu ya Serikali kama vile Mfumo mkuu wa uhasibu, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Rasilimaliwatu (HCMIS), Mfumo wa Malipo ya Serikali
Kielektroni (GePG), Mfumo wa Barua pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao na kadhalika. Aidha Moduli za Mfumo huu zinaweza kuongezwa au kupunguzwa bila kuathiri utendaji kazi wa moduli nyingine au mfumo kwa ujumla.
“Mfumo huu unasaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA, kuwezesha mifumo ya taasisi za umma kuwasiliana, kuongeza uwazi, uwajibikaji, kuaminika kwa mifumo ya Serikali na kuimarisha udhibiti wa taarifa kwa kuwa watumishi wa Serikali tu waliopo ofisini ndio watakaopata data na mafaili”, anasisitiza Dkt. Bakari.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Injinia Benedict Ndomba anaeleza kuwa katika eneo hili la mifumo tumizi, Wakala pia imetoa ushauri na msaada wa kiufundi katika taasisi 350 kwa kutengeneza mifumo tumizi ya kisekta 40 inayoboresha utendaji kazi wa taasisi, tovuti zaidi ya 400, na kutoa mafunzo kwa watumishi wa taasisi hizo katika kutekeleza jitihada za serikali mtandao. Anaeleza zaidi kuwa, Wakala ni msajili rasmi wa anuani za tovuti zenye majina yanayoishia na “.go.tz’’ inayoitambuliwa na Kituo cha Taarifa za Kimtandao Tanzania (TzNiC), ambapo kazi ya kusajili tovuti zote za taasisi za umma ikiwemo zile zilizokuwa na majina yanayoishia na .com na .org inafanyika.
Aidha, Dkt. Bakari anasisitiza kuwa maendeleo ya serikali mtandao pia yanahitaji miundombinu ya TEHAMA madhubuti, ambapo katika eneo hili Wakala imefanikiwa kusimamia ujenzi na uendeshaji wa miundombinu shirikishi ya TEHAMA kwa ajili ya matumizi ya taasisi mbalimbali za umma. Miundombinu hiyo ni pamoja na Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia simu za Mkononi (mGov) *152*00# ambao unatumiwa na Taasisi 157 ambapo huduma mbalimbali ikiwemo malipo ya Serikali (Maji, Umeme, Ardhi, ada za shule), zinapatikana kwa haraka, gharama nafuu, na kufikika kwa urahisi moja kwa moja kupitia simu yenye mtandao wowote wa simu za mkononi kama vile Tigo, Voda, TTCL, Halotel, Airtel na Zantel.
Mingine ni Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (Govnet) ambao umeunganisha taasisi 147 za Serikali kuu na Serikali za Mitaa zikiwemo hospitali na shule, na Kituo cha Serikali cha Kuhifadhi Mifumo (GDC) kinachotumiwa na taasisi za umma 53 na kuhifadhi 230. Dkt. Bakari anaainisha.
Kama ilivyo katika jitihada nyingine za maendeleo, utekelezaji wa Serikali Mtandao wenye ufanisi na endelevu unahitaji utafiti na uchunguzi wa kina ili kubaini kiini cha vikwazo vya uendeshaji na kupata ufumbuzi unaofaa na wenye manufaa kwa Serikali na wananchi, Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao Bw. Leopold shayo, anasema Wakala imeanzisha Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao kilichopo Chuo Kikuu Cha Dodoma (CIVE), kwa ajili shughuli za utafiti na ubunifu wa maendeleo ya serikali mtandao kitakachokutanisha wadau mbalimbali wenye mawazo ambayo yakiendelezwa yataleta maboresho katika jitihada za utekelezaji wa serikali mtandao katika taasisi za umma.
Aidha, Dkt. Bakari anaeleza kuwa, katika miaka saba ya utekelezaji wa jitihada hizi zote, changamoto mbalimbali zilijitokeza kama vile usalama wa mifumo na miundombinu pamoja na
taarifa zilizomo, umadhubuti wake, urudufu, rasilimali watu wenye ujuzi wa kutosha, usahihi wa matumizi na gharama kubwa za utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao. Anaendelea kueleza kuwa, masuala mengine yaliyohitaji kuwekwa sawa ni pamoja na namna ya kukabiliana na wakandarasi wa mifumo tumizi na vitumi vya aina mbalimbali kama vile kompyuta, seva na vinginevyo, ikiwemo gharama kubwa za usimikaji na usanikishaji iliyokuwa inaamuliwa kwa manufaa ya watu binafsi.
Dkt. Jabiri Bakari akihutubia washiriki kuhusu uwezo wa Mifumo ya TEHAMA inayotengenezwa nchini katika nchi zinazoendelea wakati wa Mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Athari za Kijamii za Kompyuta kwenye nchi zinazoendelea uliofanyika Dar es Salaam, tarehe 2 Mei, 2019 anasema kuwa, ni lazima izingatiwe kuwa matatizo yetu si makubwa, hivyo hayahitaji ufumbuzi unaotumia mifumo mikubwa, Ila, tunaendelea kuyafanya yawe makubwa kwa kuendelea kutumia mifumo iliyotengenezwa bila kuzingatia mahitaji halisi ya taasisi husika. Kutokana na hali hii, “tunalazimika kutumia rasilimali nyingi, kama vile fedha, muda, watu na hata miundombinu yenye uwezo mkubwa sana usio wa lazima ambao hauendani na mahitaji na mazingira halisi ya taasisi husika.” Anaeleza Dkt Bakari.
Aidha anongeza kuwa, uzoefu unaonesha kuwa michakato mingi ya utendaji shughuli za Serikali haikuungana, imekuwa migumu bila ya sababu na haiendani na mtiririko wa kawaida wa utendaji kama ilivyo na kusababisha matatizo kutokana na mazoea ya kutumia mikono. Kinachotakiwa ni kufanya jitihada ya dhati ya kufanya marekebisho ya kiufundi ya uendeshaji kazi ili kupata michakato iliyosanifiwa upya na kujumuishwa itakayoboreshwa kwa kutumia TEHAMA.
Dkt. Bakari anasema katika kipindi cha miaka saba iliyopita, Wakala ya Serikali Mtandao imefuatilia na kutengeneza mifumo na huduma mbalimbali za serikali mtandao zinazomilikiwa na Serikali kwa asilimia mia (100%). Anaendelea kusema “Sifa muhimu za mifumo yetu ya serikali mtandao ni pamoja na urahisi wake kulingana na mazingira yetu ya utendaji, gharama ndogo za uendeshaji, ukubwa wake unaolingana na ukubwa wa kazi na mahitaji na uwezo wa ndani uliyoimarishwa”.
Naye Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala Bi. Suzan Mshakangoto anasema kuwa, Wakala pia imekuwa ikishirikiana kikamilifu na wadau wake wote kama vile Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti, (Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (CoICT) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Wadau wa Maendeleo na Wananchi ili kuwa na uekelezaji madhubuti wa Serikali Mtandao nchini
Aidha Bi Suzan anasema kuwa Wakala imeendelea kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa kuandaa Vikao Kazi viwili vya mwaka vya Serikali Mtandao kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujadili njia mbalimbali za kutatua changamoto na kuleta uelewa wa pamoja wa hali ya matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma. Vikao hivyo vimesaidia kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kuzitatua changamoto za TEHAMA na kuona jinsi TEHAMA inavyoweza kutumika katika kuijenga Tanzania ya viwanda.
“Kikao Kazi cha kwanza kilifanyika Arusha kuanzia Agosti 17 hadi 20, 2015 na kilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 700 na Kikao Kazi cha pili cha Serikali Mtandao kilifanyika Januari 30 hadi Februari 2, 2019 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano na kilihudhuriwa na washiriki 786 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. Aidha taarifa zote zimekuwa zikiwekakatika tovuti ya Wakala http://www.ega.go.tz, na mitandao ya kijamii kwa jina la tzegovernmen”, anasema Bi. Mshakangoto.
“Sisi kama Wakala tutaendelea kubuni, kusanifu na kutengeneza mifumo kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani ili kukidhi mahitaji yetu halisi, tutaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA Serikalini katika maeneo mbalimbali ikiwamo eneo la usalama wa mifumo na taarifa zilizomo, tutaendea kujenga mazingira wezeshi kwa taasisi za umma ili ziweze kuwahudumia wananchi kwa kutumia TEHAMA na pia tutaendelea kushirikiana na wadau wetu wote ili kuona namna bora ya kutumia TEHAMA katika kutoa huduma kwa umma”, Dkt. Bakari anamalizia kwa msisitizo.