Home Siasa MBUNGE AKABIDHI VIFAA VYA MILIONI 7 KWA CCM MKOANI SINGIDA

MBUNGE AKABIDHI VIFAA VYA MILIONI 7 KWA CCM MKOANI SINGIDA

0
 Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida Mhe. Aysharose Mattembe (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Killimba vifaa vya ofisini vyenye thamani ya sh.milioni 7.3 alivyovitoa kwa Jumuiya  za chama hicho jana kwa wilaya zote na mkoa kwa ajili ya kusaidia kurahisisha utendaji wa kazi. Kulia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi na Kushoto ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa Mkoa wa Singida,  Yohana Msita.
 Muonekano meza kuu.
 Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Singida, Asha Mwendwa akizungumza kabla ya makabidhiano ya vifaa hivyo.
 Makada wa CCM wakiwa kwenye hafla hiyo.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa Mkoa wa Singida, Yohana Msita akizungumza.
 Mbunge Aysharose akizungumza wakati akikabidhi msaada huo.
 Makabidhiano yakiendelea.
 Hapa akimkabidhi Alhaji Killimba mafaili.

 Mbunge Aysharose Mattembe akimkabidhi Alhaji Killimba Printa.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Killimba akizungumza wakati akopokea msaada huo.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo. Kutoka kushoto ni Iddi Maalim, Martin Lissu na Diana Chilolo.
 
Na Dotto Mwaibale, Singida
 
 
MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ametoa vifaa mbalimbali vya ofisini vyenye thamani ya sh. milioni 7.3 kwa chama hicho mkoani humo ili kuwarahizishia kazi watendaji na kutunza siri za chama.
 
Akikabidhi vifaa hivyo mjini hapa jana Mattembe  alisema ametoa vifaa hivyo kwa lengo la kuwarahizishia kazi watendaji wa chama na kusaidia kutunza kumbukumbu wakati wa  uchaguzi wa serikali za mitaa.
 
” Kompyuta hizi nilizozitoa kwa chama na vifaa vingine vitasaidia kuwarahisishia kazi za kila siku pamoja na kutunza siri za kazi zetu ambazo zilikuwa zikivuja tulipokuwa tunazifanyia kwenye steshenari za nje za watu binafsi”  alisema Mattembe.
 
Mbunge Mattembe  alisema ametoa kompyuta mbili moja kwa ofisi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida na nyingine kwa ajili ya ofisi ya Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) mkoa, vifaa vingine ikiwemo printa, Stepula, mafaili, karatasi na kalamu vitapelekwa katika jumuiya za chama hicho katika wilaya zote za mkoa huo.
 
Mattembe alisema msaada wa namna hiyo alikwisha hufanya kwa kutoa kompyuta saba ambapo moja ilikabidhiwa ofisi ya CCM mkoa na sita zilipelekwa katika wilaya zote za mkoa huo na alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi na wanachama kuungana na kuwa timu moja ili kupata ushindi katika changuzi zote zijazo.
 
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya wanachama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Killimba alimpongeza Mbunge huyo kwa kuendelea kutoa misaada katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo  na kumuomba aendelee hivyo kwani chama Kinatambua mchango wake. 
 
“Chama kinatambua jinsi unavyojitoa kwa moyo wako wa dhati kusaidia wananchi katika maeneo mbalimbali hii ndio kazi ya kibunge ambayo inawafanya wananchi wakuamini na kukiamini chama chetu” alisema Killimba. 
 
Killimba alitumia makabidhiano hayo kuwaomba viongozi waliopata dhamana ya kupitisha majina ya mchujo ya wagombea uongozi wa Serikali za mitaa ndani ya CCM kutenda haki na kupitisha majina ya wagombea wanaofaa.
 
Alisema kumekuwa na baadhi ya viongozi wanashindwa kutunza mali za chama ambapo aliwataka kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwa hategemei kuona kiongozi anaomba fedha kwa ajili ya kwenda kuchapisha nyaraka za ofisi kwenye steshenari za nje.
 
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida, Yohana Msita alimpongeza mbunge huyo kwa jitihada anazo zifanya za kumsaidia Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Rais Dkt.John Magufuli kutekeleza kwa vitendo ilani ya CCM kwa kusaidia wananchi katika shughuli za maendeleo ya wananchi na chama na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo.