*******************************
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro
(MORUWASA)imevunjwa. Hatua hiyo imechukuliwa na Waziri wa Maji Mhe. Prof.
Makame Mbarawa (Mb) kuanzia tarehe 02 Oktoba, 2019.
Taarifa ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo imeainisha kuwa
kuvunjwa kwa bodi hiyo ni kwa mamlaka aliyo nayo Waziri wa Maji kwa mujibu wa kifungu Namba 14 cha Jedwali la kwanza la Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 5 ya Mwaka 2019, kikisomwa pamoja na Kanuni Na. 14 ya Kanuni za Usambazaji wa Maji (Tangazo la Serikali Na. 90 la tarehe 26/04/2019).
Taarifa hiyo imefafanua kuwa bodi ya MORUWASA imevunjwa kwa kushindwa
kutekeleza majukumu yake ya kuisimamia mamlaka ya maji hivyo kuathiri utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika manispaa ya Morogoro.
Aidha, wakati huo huo Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) ametaka kuanza kwa utaratibu utakaowezesha kuundwa kwa bodi mpya.