Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akifungua
mafunzo ya namna ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa watendaji jijini Dodoma tarehe 03 Oktoba, 2019.
Sehemu ya watendaji wa Tume ya Madini wakifuatilia hotuba ya ufunguzi iliyokuwa inatolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba (hayupo pichani) kwenye mafunzo hayo.
Mchumi Mwandamizi wa Tume ya Madini, Josephat Mbwambo akielezea namna ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tume ya Madini kwa watendaji (hawapo pichani) kwenye mafunzo hayo.
Meneja Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume ya Madini, Gift Kilimwomeshi akifafanua jambo kwenye mafunzo hayo.
********************************
Leo tarehe 03 Oktoba, 2019 Kurugenzi ya Huduma za Tume imeanza kutoa mafunzo ya namna ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa watendaji jijini Dodoma lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa namna ya kusimamia matumizi ya fedha kwenye utekelezaji wa majukumu yao. Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotarajiwa kuisha tarehe 05 Oktoba, 2019 yanashirikisha Wakurugenzi na Mameneja kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, pamoja na maafisa bajeti.
Pamoja na masuala mengine, watendaji watafundishwa masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya kuandaa taarifa za Tume ya Madini, uandaaji na ujazaji wa fomu za OPRAS, mawasiliano katika utumishi wa umma, mkataba wa huduma kwa mteja, mkakati wa uongezaji maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019/2020 pamoja na kujadili changamoto mbalimbali katika utendaji kazi.