Home Mchanganyiko VIWANDA VYA NDANI VYAPONGEZWA KWA KUWA NA UWEZO WA KUONGEZA THAMANI KOROSHO...

VIWANDA VYA NDANI VYAPONGEZWA KWA KUWA NA UWEZO WA KUONGEZA THAMANI KOROSHO YA TANZANIA

0

Hii ni picha ya meli inayopakia korosho kwenda nje ya nchi.Meli hii itabeba kontena 1015

Hiki ni kiwanda cha Amama Farmers Ltd kilichopo Tandahimba, ambapo wafanyakazi wakiendelea kubangua korosho

Katibu Mkuu Wizara ya Viwandana Biashara Prof Joseph Buchweishaija akiangalia korosho zilizobanguliwa na kiwanda cha Amama Farmers Ltd kilichopo Tandahimba kwaajili ya maandalizi ya kuwa vacummed packed ili kusafirisha njeya nchi

……………….

Dodoma-

Viwanda vya ndani nchini vimepongezwa kwa kuwa na uwezo wa kuongeza thamani korosho ya Tanzania tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipotangaza uamuzi wa Serikali kununua korosho zote za wakulima tarehe 12 Novemba, 2018.

Hayo yamesemwa na Prof. Joseph Buchweishaija, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara alipofanya ziara ya kufuatilia ubanguaji wa korosho kwenye viwanda vilivyopo Mikoa ya Mtwara na Lindi na usafirishaji wa korosho hizo nje ya nchi unaoendelea katika bandari ya Mtwara.

“Nimejionea mwenyewe korosho zetu zilivyo na ubora unaostahiki, zinabanguliwa kwa utaalam na zimefungashwa kwa kutumia vifungashio vizuri (vacuumed packed) katika madaraja yote hususan daraja la WS320 linalopendwa na wanunuaji wengi kutoka nje ya nchi. Hakika viwanda vyetu vinafanya kazi nzuri “amesema Prof. Buchweishaija.

Prof. Buchweishaija ameendelea kusema kuwa ubanguaji wa korosho uligawanyika kwa viwanda vya aina mbili yaani viwanda vidogo vinavyosimamiwa na SIDO pamoja na viwanda vikubwa. Katika kutekeleza mpango wa ubanguaji, Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) iliingia mikataba na viwanda vikubwa pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa niaba ya viwanda/wabanguaji wadogo ili kubangua korosho. Kwa viwanda vidogo kwa Mkoa wa Mtwara vilikuwa vitano ambavyo ni Siwa Food Products, Mama Vitu Super Cashewnut, Mikindani Food Processing, Akross Ltd – SIDO, Mtwara na Kitama Farmers- Tandahimba na kwa Mkoa wa Lindi vilikuwa viwanda vitatu ambavyo ni Waigero Ltd, Wabanguaji Wadogo BUCO, na Uwakoru, Ruangwa. Hadi sasa viwanda vitano vilivyochini ya usimamizi wa SIDO Mtwara ambavyo vimekamilisha ubanguaji wa korosho na viwanda viwili ambavyo ni Waigero na Uwakoru chini ya usimamizi wa SIDO Lindi vinaendelea na uzalishaji  na ubanguaji. Hadi kufikia tarehe 23 Septemba, 2019 Korosho tani 607.75 zimebanguliwa na viwanda vyetu vidogo na kuwezesha wabanguaji wadogo takribani 1,000 kupata ajira.

Kwa upande wa viwanda vikubwa Serikali iliingia mikataba na viwanda sita (6) ambavyo ni Amama Framers kilichopo Tandahimba, Perfect Cashew kilichopo Masasi, Hawte Investment kilichopo Mtwara, Al-Andalus kilichopo Lindi, Micronix kilichopo Masasi na Korosho Afrika kilichopo Tunduru. Hadi kufikia tarehe 23 Septemba, 2019 Korosho tani 3,309.64 zimebanguliwa na viwanda vikubwa na viwezezesha kutoa ajira takribani 2,511 ambao kwa asilimia kubwa ni akina mama. Hadi kufikia tarehe 23 Septemba, 2019 viwanda vinne ambavyo ni Amama Farmers, Perfect Cashew,  Hawte Investment Ltd na Al-Andalus Ltd vinaendelea na ubanguaji wakati Kiwanda cha Micronix na Korosho Afrika vimemaliza ubanguaji wa korosho ghafi kama makubaliano ya mkataba yao ambapo kwa sasa viwanda hivyo viwili vinaendelea kubangua korosho zao walizouziwa na Serikali kiasi cha tani 1,000.

Kwa upande wa usafirishaji wa korosho kutoka kwenye Ghala mbalimbali kwenda melini, zoezi linaendelea vizuri. Hadi tarehe 23 Septemba, 2019 Korosho takribani tani 40,050 zimeshapakiwa kwenye meli tayari kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara.

 “Hivi sasa ninavyozungumza tayari meli mbili zimepakia korosho na kuondoka, meli ya tatu imeanza kupakiwa ambapo itabeba kontena 1015 ambazo sawa na tani 23,328 na zoezi zima litakamilika kwa siku mbili ukizingatia kuwa kuna meli zingine mbili zipo majini na zitatia nanga na kuanza zoezi la kupakia korosho kwenda nje ya nchi” ameeleza Prof. Buchweishaija.

Alihitimisha kwa kusema kuwa zoezi la ubanguaji wa korosho zilizonunuliwa na serikali zimeweza kutoa ajira hasa kwa wanawake kwa asilimia 92 hivyo tumefanikiwa vizuri na kuonesha dalili kuwa Tanzania inaweza hasa tunapozungumzia nchi ya viwanda maana tukiuza korosho ghafi tunahamisha ajira na akatoa wito kwa viwanda kuendelea kuongeza uzalishaji ili ikiwezekana korosho zote zinazozalishwa Tanzania zibanguliwe nchini.