Home Mchanganyiko WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA KIWANDA CHA KUTENGENEZA SAMANI –VETA DODOMA

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA KIWANDA CHA KUTENGENEZA SAMANI –VETA DODOMA

0

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akielekea kwenye tukio la uzinduzi wa kiwanda cha Samani VETA Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifungua jiwe la msingi la Kiwanda cha VETA Dodoma. Pembeni ni Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Samani VETA Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akijaribu moja ya mashine katika kiwanda kipya cha samani cha VETA Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akitoa maelekezo wakati alipotembelea kiwanda cha samani cha VETA mara baada ya kukizindua rasmi

…………………..

• Ataka VETA kutumia mafundi wao kujenga Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutumia mafundi wao kujenga Vyuo 25 vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza samani cha Ufundi Stadi na Huduma cha VETA kilichopo Dodoma.

Ndalichako amesema haiwezekani VETA wakawa wanafundisha fani ya ujenzi lakini wakiwa na kazi za ujenzi wanatafuta mafundi kutoka nje.

“Kama VETA mnafundisha kujenga lazima tuone mnafanya kazi kwa vitendo sio mnataka kupaka rangi mnatafuta mafundi wa mtaani, nimesema marufuku nataka kuona hizi VETA 25 zinajengwa na ninyi wenyewe kwa kutumia mafundi wenu,” alisema Waziri Ndalichako.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kuviimarisha vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha vinatoa mafunzo bora na ya kisasa ambayo yanaendana na teknolojia ya kisasa.

“Vijana wanaotoka katika Vyuo hivi tunahakika wanakuwa na ujuzi ambao utachangia katika kujenga uchumi, ndio maana Serikali imetumia fedha nyingi tena za walipa kodi kujenga kiwanda kama hiki ili ujuzi wanaopata vijana utumike katika hatua za Uchumi wa Viwanda,”

Ndalichako pia ametoa wito kwa vijana kujiunga na mafunzo ya useremala katika chuo hicho.

“Nimeambiwa hapa na Mwenyekiti wa Bodi kwamba takwimu za wanafunzi wanaosoma mafunzo ya ufundi seremala bado ziko chini, lakini nipende kuwaambia ufundi seremala ni mzuri, kila mtu anahitaji vifaa vya ndani hivyo ni kozi ambayo inalipa. Natoa wito kwenu vijana kujiunga na mafunzo haya na niwakaribishe katika Chuo chetu cha VETA Dodoma,”
aliongeza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ameupongeza Uongozi wa VETA kwa kuweza kubuni na kutekeleza mradi wa kiwanda cha kisasa na kuwataka pamoja na kutoa mafunzo kuhakikisha wanakuwa na mpango mzuri wa uzalishaji mali utakaotumia mashine za kisasa zilizofungwa katika kiwanda hicho.

“Baada ya kuzindua kiwanda hiki nimekitembelea na kujionea namna kinavyoweza kufanya kazi kwa ufanisi, kutengeneza bidhaa kwa muda mfupi ni ukweli usiopingika kwamba kimejengwa vizuri, naamini kitazalisha samani za hali ya juu na kwa bei nafuu na kuondoa dhana kuwa samani nzuri mpaka zitoke nje ya nchi,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Juma Nkamia amesema katika nchi nyingi duniani vyuo vingi vinavyozalisha nguvu kazi ni vyuo vya VETA na kuwataka vijana wanaosoma katika chuo hicho na wale walio nje ya chuo hicho kutoa hamasa kwa watanzania kusoma kwenye vyuo vya VETA ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Peter Maduki amesema kiwanda hicho kitaendelea kuzalisha samani zenye ubora na nafuu zinazoendana na mahitaji ya soko na kwamba uwepo wa Kiwanda hicho utasaidia kuongeza mapato ya Taasisi.

Maduki alimweleza Waziri kuwa katika kufanikisha hilo watahakikisha wanaweka Menejimenti itakayoweza kuendesha kiwanda hicho na kuona malengo yaliyowekwa yanafikiwa huku akiongeza kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika vyuo vya Veta ni kushindwa kupata wanafunzi wa kutosha wa fani ya useremala.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Pancras Bujulu alimweleza Waziri Ndalichako kuwa ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji samani Dodoma umetekelezwa kwa awamu mbili, ya kwanza ikiwa ya ujenzi wa jengo na miundombinu yake na awamu ya pili ikiwa ununuzi na ufungaji wa mashine na mitambo, kazi zote zikigharimu zaidi ya shilingi bilioni 3 ambazo ni fedha za ndani.

Hafla ya ufunguzi wa Kiwanda cha kutengeneza samani VETA Dodoma imekwenda sambamba na mahafali ya 36 ya Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma.