***************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WENYE Viwanda 173 mkoani Pwani wamethibitisha kushiriki katika maonyesho ya pili ya viwanda yanayotarajiwa kufanyika octoba 17-23 mwaka huu ,idadi ambayo bado ni ndogo kukidhi lengo la washiriki 400 lililokuwa limewekwa kimkoa.
Aidha waliothibitisha kushiriki katika kongamano la wawekezaji ni 170 ,hivyo mkoa unaendelea kuwaomba wawekezaji kujitokeza na kuchangamkia fursa hiyo .
Akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na tathmini ya maandalizi ya maonyesho na kongamano hilo ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema , kamati imependekeza kusogeza mbele maonyesho hayo ambapo yatakuwa octoba 17 hadi 23 badala ya tarehe 1-7 octoba .
Alieleza, kati ya washiriki waliojitokeza 53 ni viwanda ,wajasiriamali 100 na wenye viwanda vidogo (SIDO ) 20 ikiwa ni chini ya asilimia 50.
Pamoja na hilo ,Ndikilo alifafanua wanatarajia kuongeza idadi ya wawekezaji watakaoshiriki kutoka 166 mwaka 2018 hadi kufikia 500.
“Pia inatupasa tupishe maandalizi kuelekea siku ya kuzima mwenge ,na baada ya hapo ndipo kutafanyika maonyesho na kongamano hili”
“Waratibu wa maonyesho hayo watakuwa ni wabobezi wa masuala ya maonyesho kama hayo kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) pamoja na mamlaka ya maendeleo ya viwanda (TANTRADE)”
Alieleza, malengo ya matukio hayo ni kuonyesha kwamba mkoa wa Pwani ,umedhamiria kuwa ukanda wa viwanda,wenye viwanda kupata masoko ya uhakika,kupanua wigo wa soko la ndani ya mkoa kufikia kimataifa na ,kuvutia wawekezaji wapya.
Aidha Ndikilo alifafanua lengo la kongamano hilo ,kuwa ni kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo utalii,uchumi,kijamii,kilimo,uvuvi na viwanda.
“Kufanyika kwa kongamano hili italeta picha halisi ya fursa zote zilizopo mkoani Pwani,na kuonyesha namna mkoa ulivyopiga hatua katika sekta ya viwanda,uwekezaji na fursa za miradi mikubwa ikiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa uzalishaji umeme megawatts 2,100 STIGO ,huko Rufiji”alibainisha Ndikilo.
Nae Januarius Maganga wa TSN alisema ,wanakwenda kuratibu maonyesho hayo ikiwa ni maonyesho ya kumi .
Kwa upande wake ,mwakilishi wa mkurugenzi kutoka TANTRADE ,Victor Rugemalila aliwahakikishia wananchi na mkoa kwamba ,wamejipanga kuona namna bidhaa inakua na kuleta maendeleo ya wenye viwanda na kuratibu kwa ufanisi mkubwa maonyesho hayo.