***************************
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba, ameanzisha ligi ya Mpira wa miguu ya “ Uchaguzi Cup” yenye lengo la kuhamasisha wananchi, kujiandikisha na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, utakaofanyika novemba 24 mwaka huu.
Ligi ya “ Uchguzi cup ” inafanyika katika viwanja vya michezo vya mbamba-bay na Kilosa Wilayani hapa na inashirikisha timu kumi na tatu (13) za mpira wa miguu za wilayani hapa.
Akifungua Ligi hiyo, jana katika uwanja wa Polisi Mbamba-bay wilayani hapa Bi Chilumba, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kujitokeza kwa wingi katika michezo ya ligi hiyo, kwa kuwa watapata burudani ya mpira wa miguu bila kiingilio chochote.
Alifafanua kuwa, lengo la mashindano ni kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu kwa kuwachagua viongozi wa Vijiji na Vitongoji.
Bi Chilumba aliongeza kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni wa muhimu sana kwa kuwa viongozi hawa ndio wanaoishi moja kwa moja na wananchi na wanatoa maamuzi kwa ngazi za Serikali za Mitaa hivyo wananchi wanatakiwa kuhamasika, na kuwachagua vongozi wanaowafaa.
Alitoa wito maalum kwa vijana kujitokeza kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za mitaa kwa kuiga mfano wa Mh.Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli kwa
kuwa Teuzi nyingi anazozifanya zinajumuisha vijana wengi.
Mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo ulizikutanisha Timu za Likwilu fc na Linda Fc na matokeo timu hizo zilikwenda suluhu ya magoli mawili kwa mawili.