WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi Wilayani Mlele Mkoani Katavi, jana. Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuwahamisha askari wote wa Kituo cha Polisi Majimoto kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili askari hao. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Zuberi Homera.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi Wilayani Mlele Mkoani Katavi, jana. Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuwahamisha askari wote wa Kituo cha Polisi Majimoto kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili askari hao. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Zuberi Homera. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………
Na Felix Mwagara, MOHA-Katavi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Katavi, kuwahamisha askari wote wa Kituo cha Polisi Majimoto kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili askari hao.
Waziri Lugola alitoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Mji wa Majimoto, Wilaya ya Mlele wakati akijibu kero mbalimbali za wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Lugola alisema kero zilizowasilishwa na wananchi hao, zinaonyesha askari wa kituo hicho wanajihusisha na vitendo mbalimbali vya rushwa, kupiga wananchi ovyo, kushindwa kudhibiti ulinzi na usalama pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi.
“Natoa agizo hili liwe fundisho kwa askari wote wasiowaaminifu kote nchini, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huu natoa siku saba askari wote wa kituo hiki wahamishwe na waletwe wengine ili wajifunze,” alisema Lugola.
Baada ya agizo hilo, waendesha bodaboda na wananchi wengineo, walishangilia na kusema kuwa mji huo sasa utatulia kutokana na uwepo wa amani bila kuwa na manyanyaso.
Mmoja wa wananchi aliyetoa malalamiko dhidi ya polisi katika kituo hicho ni Malewe Maswe, alilalamikia kuwa baadhi ya askari hao walimpiga na kumsababishia maumivu makali ya miguu kutokana na kuhoji kosa lake la kuletwa kituoni hapo baada ya kugombana na mwalimu mmoja katika mji huo.
“Tulikuwepo na Mwalimu niliyegombana naye kituoni hapo, askari wakaniambia nendeni mkaelewane na mwalimu huyo, nikawaambia hatuwezi elewana maana zoezi hilo lilishindikana, askari wakasema unatufundisha kazi, yule pale dogo (askari ambaye alikuwa katika mkutano huo) simjui jina lake alinipiga kipigo sana, na askari mwingine bonge anachochea hii ndiyo Serikali ya Magufuli,” alisema Maswe.
Aidha, Waziri Lugola alijibu kero mbalimbali, ikiwemo ya Mkazi wa Mji huo, Malugu Mayombi ambaye ni mkulima maarufu wa mpunga wa eneo hilo, aliangua kilio kwa waziri akidai polisi wameshindwa kushughulikia kesi yake ya madai ya shilingi milioni sitini (6000,000/-) anazomdai mfanyabiashara Sali Kulwa maarufu TBS aliyemuuzia gunia 623 za mpunga.
“Waziri wangu, naomba unisaidie mimi maskini, ujiowako utaniokoa, nakuomba Waziri unisaidie nadai shilingi milioni 33 na laki 5 kati ya shilingi milioni 60 nimelipwa shilingi milioni 26 na laki 5 pekee, nimeshindwa kuendeleza kilimo naishi kwa shida, nilikuwa nalima ekari 100 kwasasa nalima ekari 30 tu nisaidie jamani, nateseka mimi,” alisema Mayombi.
Waziri Lugola alimuagiza Kamanda wa Polisi kushirikiana na Mkuu wa Polisi Wilaya kulitatua suala hilo kwa muda wa wiki moja wamkamate mtuhumiwa na aweze kumlipa fedha za Mayombi.
Waziri Lugola amemaliza ziara ya siku tano Mkoani Katavi, na ameelekea Mkoani Rukwa kuendelera na ziara ya kikazi akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika mikutano mbalimbali ya hadhara mkoani humo.