Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba Bw.Akida Khea akiongea na Wanahabari baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya Wakaguzi wa Dawa wa Mkoa wa Pwani na TMDA Kanda ya Mashariki.
Washiriki wa Mafunzo ya Wakaguzi wa Dawa wakifuatilia mjadala baada ya kufunguliwa Mafunzo hayo leo Wilayani Kibaha.
**************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wakaguzi wa dawa Pwani na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza jukumu lao kuepukana na uwepo katika soko la bidhaa duni na bandia katika maeneo yao ya kazi na hivyo kuwaepusha wananchi na madhara kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.
Ameyasema hayo leo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Gunini Kamba katika Ufungunzi wa Mafunzo ya Wakaguzi wa Dawa Mkoa wa Pwani na TMDA kanda ya Mashariki Wilayani Kibaha.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Dkt.Kamba amesema kuwa mafunzo wanayoyapata Wakaguzi hao yatawaelimisha kuhusiana na jukumu lao la kuwezesha mazingira mazuri na kuhamasisha ongezeko la uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchinibpamoja na biashara kwa ujumla.
“Katika mafunzo haya wakaguzi watakumbushwa juu ya maadili ya kazi ya wakaguzi wa dawa, sifa za mkaguzi wa dawa, kuelezwa wajibu wao kama wakaguzi, sheria na mabadiliko yake yaliyopelekewa kuwepo kwa taasisi ya TMDA kutoka TFDA, kanuni na miongozo ya utendaji kazi inayowahusu wakaguzi wa dawa”. Amesema Dkt.Kamba.
Aidha Dkt.Kamba amesema kuwa Mkoa wa Pwani umekuwa mstari wa mbele nchini katika kuvutia uwekezaji wa viwanda na hususani vya dawa.
“Mpaka sasa , tayari tuna viwanda vya dawa sita(6) ambavyo vimeanza kujengwa tangu serikali ya awamu ya tano ilivyoingia madarakani”.Amesema Dkt.Kamba.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba Bw.Akida Khea amesema kuwa hadi sasa zaidi ya 80% ya dawa zinazotumika hapa nchini zinatoka nje ya nchi pamoja na kwamba udhibiti katika vituo vya forodha na katika soko umeimarishwa .
“Bado kuna changamoto ya uwepo wa dawa duni, bandia na ambazo hazijasajiliwa. Dawa hizi hazina budi kufuatiliwa na kuondolewa kwenye soko”.Amesema Bw.Khea.
Pamojaa na hayo Bw.Khea amesema kuwa Mamlaka inahitaji wakaguzi wenye weledi katika kutambua dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi pamoja na kuhamasisha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini.