Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetoa mafunzo ya ukaguzi wa mizigo kwa kutumia teknolojia ya Nyuklia kwa wafanyakazi 22 wa Kitengo cha Midaki (scanner) katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yamelenga kuwapa uwezo wafanyakazi wanaoshugulikia ukaguzi wa mizigo katika midaki (Scanner) katika eneo la Bandari kwa lengo kuongeza kasi na weledi katika ufanyaji kazi kwa lengo la kuharakisha ukaguzi wa mizigo Bandarini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Prof Lazaro Busagala amewataka wafanyakazi hao kuhakikisha kuwa wanafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa lengo la kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa mizigo kwa njia ya teknolojia ya Nyuklia.
“Hakikisheni mnatumia mafunzo haya katika kufanya kazi kwa weledi na kuongeza tija ili kusiwe na ucheleweshwaji wa mizigo hapa bandarini” alisema Prof Busagala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Midaki (Sscanner) Bandarini, Bw. Mtani Rugina amesema kuwa wataendelea kuhakikisha wafanyakazi wote waliopo kwenye maeneo ya ukaguzi wa mizigo bandarini hapo wanapata mafunzo ili kuboresha ufanisi katika ufanyaji kazi wao.
TAEC itaendelea na jukumu lake la kutoa mafunzo ili kuhakikisha usalama katika maeneo yote yenye vyanzo vya mionzi unakuwa wa kiwango cha juu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala, akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya uchunguzi wa mionzi kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala (wa pili kushoto), akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya uchunguzi wa mionzi, Frank Mwamakula, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Mafunzo hayo yametolewa leo na Tume hiyo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.