Na Silvia Mchuruza ,Kagera;
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza maandalizi ya uchaguzi mkoani kagera ambapo imekutana na Wadau wa Uchaguzi na kutoa maelekezo juu ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura.
Akizungumza na wajumbe wa uchaguzi Mkurugenzi kutoka tume ya Taifa ya uchaguzi Bi. Asina Omari ametaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni kutoa taarifa juu ya kukamilika kwa maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura.
“Napenda kuwajulisha kuwa uzinduzi rasmi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura umekwisha fanyika siku ya tarehe 18 julai 2019 mkoani Kilimanjaro na baada ya zoezi huo zoezi hili limeendelea kufanyika katika mikoa ya Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Geita, na Shinyanga kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi” alisema Bi.Asina.
Bi Asina ameongeza kuwa mpaka sasa Tume imekamilisha sehemu kubwa ya maandalizi ya Uboreshaji ikiwa ni pamoja na uhakiki wa vituo vya kujiandikisha, uandikishaji wa majaribio, maandalizi ya Vifaa vya Uboreshaji wa Daftari, Mkakati wa Elimu ya mpiga kura, uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura n.k uboreshaji huo utafanyika kwa kutumia mashine ya kielektroniki ya Biometriki (BVR).
Mkutano huo umehusisha Viongozi wa vyama Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za kiraia, wawakilishi wa makundi maalum ya watu wenye Ulemavu,na wanahabari kutoka mkoani kagera.