****************************
BUKOBA
Halmashauri ya Bukoba iliyoko wilayani Bukoba mkoani Kagera kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la TADEPA limeanza kampeini maaalum ya upimaji wa ugonjwa wa UKIMWI kwa vijana kufuatia kundi hilo kuwa na mwitiko duni katika mazoezi mengine ya upimaji.
Mganga mkuu wa halmashauri hiyo Dr,Gandoch Gabriel amesema kuwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi yamepanda kwenye halmashauri hiyo kutoka asilimia 4 hadi 6 na kwamba pamoja na kuwapima vijana inatolewa elimu juu ya ugonjwa huo ili kuepusha maambukizi ya ugonjwa huo kuendelea kuongezeka.
Amesema kuwa inapobainika uwepo wa kijana yeyote mwenye maambukizi ya virus vya ukimwi uanzishiwa dawa za kufubaza virus hivyo na kwamba sambamba pamoja na upimaji wa ukimwi kampeini hiyo inaambatana na upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake ugonjwa wenye mahusiano makubwa na UKIMWI.
Kwa upande wao baadhi ya vijana wa tarafa ya Rubafu iliyoko halmashauri ya Bukoba wamesema kuwa wengi wao wamekuwa wakiogopa kupima kutokana na kutokuwa na elimu juu ya ugonjwa huo na kwamba kampeini hiyo imewawezesha kufahamu afya zao na elimu ya UKIMWI.
Hata hivyo kampeini hiyo ilihusisha ligi ya mpira ambayo imewezesha kuwakutanisha vijana wengi ambao wengi wao wameweza kupima afya zao kwa ushawishi kupitia michezo kama mpira wa mguu.