Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Asia Ngalison akizungumza kwenye mahafali ya nane ya shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani, kulia ni Mkurugenzi wa shule hiyo Mchungaji Sommy Severua na kulia kwake ni Ofisa elimu msingi Simanjiro Silvanus Tairo na mwalimu mkuu Tumaini Mbise.
Wanafunzi wa darasa la sita wa shule ya awali na msingi New Light wakicheza gwaride katika mahafali hayo.
Baadhi ya wahitimu wa darasa la saba wa shule ya awali na msingi New Light wakiwa kwenye mahafali ya nane ya shule hiyo.
………………
JAMII Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetakiwa kuhakikisha inapambana na tatizo la mimba za utotoni kwa kuwasomesha watoto wa kike na siyo kuwaozesha wakiwa wadogo.
Ofisa maendeleo ya jamii wa wilaya ya Simanjiro, Asia Ngalisoni ameyasema hayo jana kwenye mahafali ya nane ya darasa la saba ya shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani.
Ngalisoni alisema wanatakiwa kupambana nalo kwani baadhi ya watoto wa kike wanaachishwa masomo na wazazi na walezi wao kutokana na kuozeshwa wakiwa wadogo kwa tamaa ya mali.
Alisema tatizo la mimba za utotoni zinaweza kukomeshwa kwa ushirikiano wa wazazi na walimu kwani mtoto akikatishwa masomo watatoa taarifa sehemu husika.
Ofisa elimu msingi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Silvanus Tairo aliitaka jamii kusomesha watoto wao kwani kuna baadhi ya shule wanafunzi hawahitimu hata darasa la saba.
Tairo alisema shule ya msingi Lerumo ilikuwa na wanafunzi 20 walioanza darasa la kwanza na mwaka jana waliandikisha wanafunzi sita wakufanya mtihani wa darasa la saba ila wakafanya wanafunzi watatu.
Mkurugenzi wa shule hiyo mchungaji Sommy Severua alisema elimu ina nguvu mno kwani inaweza kusababisha mtoto wa kibarua akawa daktari bingwa.
“Mtoto wa kibarua anaweza kuwa bosi kutokana na ukubwa wa elimu aliyonayo hivyo tunapaswa kuzingatia hilo kwa kuwapatia elimu watoto wetu,” alisema mchungaji Severua.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Tumaini Mbise alisema wanafanya vyema kitaalamu kwani mwaka jana katika mtihani wa darasa la saba walishika nafasi ya kwanza kiwilaya na nafasi ya sita kimkoa.
Mbise alisema hata kwenye suala la maadili wanafanya vyema kwani kuna wanafunzi waliwapokea wakiwa wakorofi lakini hivi sasa ni watiifu.
Katibu wa shule hiyo, Oscar Gunewe alisema New Light ni ya kutwa na bweni ilianzishwa mwaka 2006 na inamilikiwa na kanisa la Pentekoste.
Gunewe alisema shule hiyo ina wanafunzi 546 wavulana 256 na wasichana 290 wakiwemo yatima na familia zisizojiweza 20 ambao hawatozwi ada.
Mmoja kati ya wazazi wenye wanafunzi waliohitimu, Stella Sumary aliwashukuru walimu na uongozi wa shule hiyo kwa elimu wanayoitoa kwa wanafunzi wao.