Home Mchanganyiko WATUMISHI WA UMMA KATIKA HALMASHAURI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA WELEDI

WATUMISHI WA UMMA KATIKA HALMASHAURI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA WELEDI

0

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro  akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara na  Kilombero (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

Watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Ifakara na  Kilombero wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani)  wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini..

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyesimama)  akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara na  Kilombero (pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

……………..

Na. Aaron Mrikaria

Watumishi wa umma  wanaofanyakazi makao makuu ya  Halmashauri za Wilaya nchini wametakiwa kutofanyakazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia  weledi, ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wanaowahudumia na  watumishi wenzao wanaotoka pembezoni kufuata huduma wilayani.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean  Ndumbaro wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Kilombero,Ifakara Mji na Malinyi kwa nyakati tofauti,  ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

Dkt. Ndumbaro amewasisitiza watumishi hao, kuhakikisha wanawahudumia vizuri watumishi wa umma  wanaotoka kwenye kata, tarafa na vijiji ili nao waweze kuwahudumia vizuri wananchi katika maeneo yao ya kazi.

“Hatuna budi kuwahudumia ipasavyo wananchi na watumishi wanaotumia gharama zao kufuata huduma wilayani sanjari na kupoteza muda wao, tusiwaache waondoke bila kupata huduma inayostahili” amesema Dkt. Ndumbaro.

Aidha  Dkt. NDUMBARO amewashauri watumishi wanaotaka kusoma shadada ya pili wabobee katika fani zinazoendana na shahada ya kwanza kwakuwa shahada ya kwanza ndio msingi wa taaluma walizonazo,  na endapo mtumishi atajiendeleza kwa kuchukua shahada ya pili tofauti na ya kwanza atakuwa amejiendeleza katika kada tofauti hivyo kukosa fursa ya kubadilishiwa cheo (recategorization) na kukosa sifa ya kupata kibali cha mshahara binafsi.

Dkt. Ndumbaro amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Ifakara Mji na Malinyi kuhimiza uwajibikaji, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) aliyemtaka kuchunguza weledi wa utendaji kazi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.