NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
VITONGOJI Sita vilivyopo maeneo ya uwekezaji kata ya Zinga pamoja na RAZABA kata ya Makurunge eneo la serikali alilopewa mwekezaji BAKHRESA kwa ajili ya uwekezaji wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani vimefutwa kwa mujibu wa sheria na havitoshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
Vitongoji hivyo ni Kikonga ,Kasiki ,Pande ,Mkunguni, Mbegani vilivyopo kata ya Zinga eneo la EPZA na RAZABA kata ya Makurunge .
Akizungumza katika baraza la madiwani, Bagamoyo mkuu wa wilaya hiyo, Zainab Kawawa aliwaasa madiwani na viongozi kwenye maeneo hayo wasijiingize katika ushabiki wowote kutokana na maamuzi hayo ya serikali ambayo ni ya msingi na yenye nia njema.
Alieleza ,vitongoji hivyo vimefutwa na Tume ya Uchaguzi ,na mchakato huo ulianzia chini ,msije kukosoa na kupingana na serikali na kushirikiana na wananchi ambao wameshaanza kunung’unika .
“Uchaguzi unatarajiwa kuwa Novemba 24 mwaka huu, madiwani mtoe ushirikiano katika maandalizi ya uchaguzi huo ,ili kupata viongozi bora,”
“Msipange safu ,kwani itasababisha kupata viongozi wasio bora,tunataka uchaguzi uwe huru na wa haki na usio na chembe ya rushwa”alifafanua Zainab .
Nae msimamizi wa uchaguzi , wilaya ya Bagamoyo, Malboard Kapinga alieleza kwamba, uchaguzi huo hautohusisha vitongoji hivyo sita kutokana na wananchi kulipwa fidia kwenye maeneo ambayo yapo katika uwekezaji na walitakiwa kuondoka.
Kapinga alibainisha ,bajeti ya uchaguzi itagharimu takriban milioni 200 ambapo serikali kuu itatoa milioni 163 na halmashauri milioni 54 na hadi sasa serikali kuu imeshatoa milioni 119 na halmashauri milioni 27.
“Elimu ya uraia tunatarajia kuendelea kuitoa mwezi octoba katika maeneo yote vitongoji 167 na vijiji nane na vifaa vya uchaguzi vimeanza kuandaliwa”aliweka bayana.
Awali diwani wa viti maalum kata ya Yombo Elizabeth Shija alilitaka kundi la wanawake kujitokeza kushiriki kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi na kuwaasa kuthubutu bila uoga ili kufikia 50 kwa 50.
Diwani wa kata ya Yombo ,Muhammed Usinga alisema wamejipanga na tayari wamehamasisha wanaCCM kuanzia ngazi ya tawi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wakazi.
Alisema ,hakuna asiyekosa macho ama kusikia ,utekelezaji wa ilani ya CCM umetekelezeka kwa asilimia kubwa chini ya Rais dkt.John Magufuli na hakuna wakumpinga kutokana na juhudi zake za kuinua maendeleo na uchumi kijumla.
Usinga ,aliwaomba wananchi wasifanye makosa katika uchaguzi huo na uchaguzi mkuu 2020 ,wachague CCM ili kuendelea kula matunda .