Picha ya Pamoja ikiongozwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sambamba na Watoa Huduma za Afya na Watumishi wa Sekta ya Afya baada ya kumaliza Semina ya mafunzo juu ya njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa (Maambukizi) kwa kufuata kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC guideline), Jijini Dar es salaam.
Afisa kutoka Kitengo cha Uhakika Ubora Wizara ya Afya Dkt. Joseph Hokororo akitoa mafunzo mbele ya Watumishi wa Sekta ya Afya wakati wa Semina ya mafunzo juu ya kujikinga dhidi ya Maambukizi kwa kufuata miongozo yakutoa huduma kwa mgonjwa (IPC guideline).
Bi. Laura Marandu, Afisa kutoka Kitengo cha Uhakika Ubora Wizara ya Afya akitoa mafunzo ya jinsi yakumkinga kichanga dhidi ya maambukizi mapya kwa kufuata miongozo ya IP.
*******************************
Na WAMJW – DSM
Watu zaidi ya milioni.1.4 duniani wanaugua magonjwa yanayosababishwa na kupata maambukizi mapya wakati wa kupata huduma.
Hayo yameelezwa na Afisa kutoka kitengo cha Uhakiki Ubora Wizara ya Afya Dkt. Joseph Hokololo wakati wa mafunzo njia ya kujikinga dhidi ya Magonjwa (Maambukizi) kwa kufuata kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa, katika maeneo ya utoaji huduma yaendelea Jijini Dar es salaam, ikiwa ni moja kati ya mikoa iliyo katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Ebola kutokana na muingiliano wa watu kutoka nchi mbali mbali
Dkt.Hokololo alisema kuwa maambukizi hayo hutokana na watoa huduma za afya afya kutofuata taratibu za namna ya kutoa huduma.
Katika mafunzo hayo ambayo yametolewa na Kitengo cha Uhakiki Ubora, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa timu za uendeshaji huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na za Halmashauri (CHMTs) za Mkoa wa Dar es salaam
“Timu za uendeshaji huduma za Afya mnatakiwa kusimamia miongozo ya kukinga na kudhibiti maambukizi (Magonjwa) wakati mnatoa huduma za Afya kwa Wagonjwa ili kudhibiti maambukizi mapya”Alisisitiza Dkt.Hokololo
Aliendelea kusema kuwa Asilimia 15 ya Wagonjwa hupata maambukizi ya magonjwa mapya pindi waendapo kupata huduma za Afya katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya, kutokana na kutofuatwa kwa miongozo ya kutoa huduma za Afya (IPC Guideline, SOP).
Aidha, Dkt. Hokororo amesema kuwa Tanzania ipo kwenye hatari ya kupata wagonjwa wa Ebola kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na ukaribu na Nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ambako Mlipuko unaendelea.
Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania tayari imekwisha kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa huo ili kuhakikisha hauingii nchini, ikiwemo kuelimisha jamii njia za kujikinga na Ugonjwa ili kuzuia usiingie nchini, na kutoa Elimu kwa Watoa huduma za Afya juu ya kumuhudumia mtu mwenye dalili za Ebola endapo atatokea.
Kwa upande mwingine, Afisa kutoka Kitengo cha uhakika ubora Wizara ya Afya Bi. Laura Edward Marandu amesema kuwa kufuata miongozo ya utoaji huduma katika vituo vya kutolea huduma za Afya kusaidia kupunguza vifo vya vichanga pindi vinapozaliwa kwa kuvikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa yanayohusiana na sehemu za kutolea huduma za Afya (Health care associated infections)
Naye Mtaalamu wa Maabara kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi MUHAS Bw. Akili Mawazo Mwakabhana amesema kuwa kutofuata miongozo ya IPC ni moja ya chanzo kikubwa cha ongezeko la maambukizi ya magonjwa yanayopatikana katika vituo vya kutolea huduma (nosalcomial diseases)
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Medipeace, yanatarajia kuendelea katika mikoa yote iliyo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Ebola ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.