Home Mchanganyiko WAZIRI HASUNGA AIAGIZA TFRA KUHAKIKISHA MBOLEA INAPATIKANA KWA BEI NAFUU

WAZIRI HASUNGA AIAGIZA TFRA KUHAKIKISHA MBOLEA INAPATIKANA KWA BEI NAFUU

0

Sehemu ya washiriki wa mkutano wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga wakati akifunga mkutano mkuu wa Wakala wa usambazaji wa mbolea Tanzania (TADCOs) katika ukumbi wa Polisi Jamii Jijini Dodoma jana tarehe 18 Septemba 2019. 

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akifunga mkutano mkuu wa Wakala wa usambazaji wa mbolea Tanzania (TADCOs) katika ukumbi wa Polisi Jamii Jijini Dodoma jana tarehe 18 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akifunga mkutano mkuu wa Wakala wa usambazaji wa mbolea Tanzania (TADCOs) katika ukumbi wa Polisi Jamii Jijini Dodoma jana tarehe 18 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
***************************

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati na bei nafuu.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameyasema hayo jana tarehe 18 Septemba 2019 wakati akifunga mkutano mkuu wa Wakala wa usambazaji wa mbolea Tanzania (TADCOs) katika ukumbi wa Polisi Jamii Jijini Dodoma.

Mhe Hasunga amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti uwepo wa pembejeo feki nchini.

Alisema Kwa upande wa mbolea, tayari Wizara ya Kilimo imetoa mafunzo na kuwapitisha Wakaguzi 50 wa mbolea ambao wanaenda kuongeza nguvu kwa kufanya kazi nchi nzima za kudhibiti ubora wa mbolea.

Mhe Hasunga alisema kuwa kwa upande wa Viuatilifu, ameiagiza Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu ukanda wa Kitropiki (TPRI) kuhakikisha wanafanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini na kuondoa viuatilifu feki vyote sokoni.

Aidha, tayari Wizara imeridhia na kuwapitisha Wakaguzi (Inspectors) 45 wa kukagua viuatilifu ambao nao wanaenda kuongeza nguvu nchi nzima kuhakikisha tatizo la viuatilifu feki linamalizika.

Kadhalika Mhe Hasunga amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kudhibiti na kuondokana na changamoto ya uwepo wa pembejeo ambazo hazikidhi viwango.

Katika mkutano huo Mhe hasunga ameupongeza uongozi wa TADCOs kwa mwanzo mzuri wa kiuongozi hususani kuwasomea wananchama wao mapato na matumizi hukuakitoa rai kwa Viongozi wote, kuhakikisha wanaendesha chama hicho kwa ufanisi mkubwa, uwazi na uwajibikaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ushirika nchini.

Aliongeza kuwa ana matarajio kwamba, kuanzishwa kwa chama hicho cha Ushirika kutapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwepo na kusaidia kuwanufaisha wakulima kwa kuagiza na kusambaza  pembejeo zenye ubora, kwa wakati na bei nafuu.

“Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwakomboa wakulima nchini kwa kuhakikisha wanazalisha mazao yao kwa tija ili waweze kuinua hali zao za maisha na kuchangia uchumi wa nchi.  Ni ukweli usiopingika kuwa azima hii hawezi kufikiwa kama wakulima hawatapata pembejeo zenye ubora, kwa wakati na kwa bei nafuu” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Dhamana mliyonayo  ni kubwa sana, hivyo ni matarajio yangu kuwa mtatimiza jukumu lenu kuu la kuhakikisha mnasimamia usambazaji wa pembejeo za kilimo wakulima wa Tanzania walio wanyonge kwa uaminifu na uweledi mkubwa.”

Aliwataka (TADCOs) kufuata Sheria, kanuni na taratibu zote zinazohusu uendeshaji wa biashara ya pembejeo nchini na kuzingatia kanuni za ushirika.  Aidha, kushirikiana na Taasisi zote zinazodhibiti na kusimamia tasnia ya pembejeo na ushirika nchini kama vile TFRA, TPRI, ASA, TOSCI, TCDC na TFC ili waweze kuwasaidia wakulima kupata pembejeo zenye ubora.

Ili kupunguza gharama na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo sahihi, kwa wakati na bei nafuu, Mhe Hasunga aliwaagiza Viongozi wenu wa TADCOs kusimamia vilivyo zoezi la uagizaji wa pembejeo kwa pamoja, moja kwa moja kutoka viwandani na si kwa wauzaji wa kati.