Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc, Bw. Ali Mufuruki (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa mwaka wa wanahisa wa Vodacom uliofanyika jijini Dar Es Salaam leo. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Hisham Hendi (kushoto) na Mkurugenzi wa Fedha Jacques Marais.
Mkuu wa Mipango na Uwekezaji wa Vodacom Tanzania Plc, Hilda Bujiku akizungumza na wanahisa waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa Vodacom Tanzania jijini Dar Es Salaam leo.
Sehemu ya wanahisa waliojitokeza kwenye mkutano wa mwaka wa Vodacom Tanzania Plc uliofanyika jijini Dar Es Salaam leo.
*******************
Kampuni ya mawasiliano ya simu za mikononi inayoongoza Tanzania,
Vodacom Tanzania PLC imetangaza faida ya mwisho wa mwaka
ya kiasi cha TZS bilioni 90.2 kwa mwaka wa fedha 2018/2019
ulioishia mwezi Machi mwaka huu.
Wakati huo huo Kampuni ya Vodacom ambayo ina mtandao
wenye kasi zaidi nchini inajivunia thamani iliyojitengenezea katika
kipindi cha miaka ya hivi karibuni ikiwemo TZS bilioni 54.5
ambazo zimelipwa kama gawio kwa wanahisa.
Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa mapato
yatokanayo na huduma ambayo yanafikia TZS bilioni 1018.9,
ambayo yamesababishwa na kukua na kuimarika kwa mapato
yatokanayo na huduma za M-pesa, ununuzi wa Intaneti (Bando)
na mapato yatokanayo na ujumbe wa simu. Kampuni ya
Vodacom imepata wateja wapya wapatao milioni 1.2 katika
mwaka huu wa fedha jambo ambalo linaongeza idadi yake ya
wateja kufikia milioni 14.1.
Katika mwaka huu wa fedha kampuni ya Vodacom ilifanya
uwekezaji mkubwa wa zaidi ya TZS bilioni 171.4 sawa na
(asilimia 16.7% ya Mapato) katika kupanua mtandao wake,
kuongeza maeneo yanayopata mtandao wa 4G katika miji
mikubwa nchini, kuongeza uwezo na kuboresha mtandao kuweza
kutoa huduma ya data ya kiwango cha juu kwa wateja.
Wakati huo Shilingi bilioni 59 zimewekezwa katika mishahara,
mafunzo na maendeleo ya wafanyakazi wake wa kudumu
wapatao 548 pamoja na kutoa ajira isiyo ya moja kwa moja kwa
zaidi ya Watanzania 127,000.
Akiongea katika mkutano mkuu wa mwaka wa kampuni ya
Vodacom leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni
ya Vodacom bwana Ali A. Mufuruki amesema, “Kampuni ya
Vodacom vile vile inajivunia uwekezaji wake katika jamii ambao
una thamani ya jumla ya shilingi trilioni 1.1, ambazo ni fedha
zilizochangiwa katika uwezeshaji wa jamii kupitia kodi, ada za
udhibiti katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambapo malipo ya
zaidi ya Shilingi trilioni 0.4 yalifanyika katika mwaka 2019 peke
yake.”
“Ukuaji katika sekta ya mawasiliano imekuwa wa pole pole katika
kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Tukiwa kama watendaji
muhimu katika sekta hii, tunajivunia kuwa chanya katika ukuaji wa
sekta hii,” alihitimisha bwana Mfuruki.