Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya benki ya NMB leo wakati alipoelezea namna Benki ya NMB na Benki ya Kilimo TADB zinavoshirikiana katika kumkombo mkulima wa Korosho kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Filbert Mponzi.
Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Filbert Mponzi wakati akielezea namna benki hiyo ilivyowakopesha wakulima wa zao la Korosho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine akielezea jinsi benki ya TADB itakavyotoa dhamana ya asilimia 50 ya mkopo kwa benki ya NMB ili iweze kuwakopesha wakulima wa Korosho.
……………………………………………………
BENKI ya NMB kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imedhamiria kumwinua mkulima wa korosho kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine alisema kuwa ili kuchochea kilimo maendeleo sekta ya kilimo wameshirikiana na benki ya NMB ambayo itatoa mikopo kwa wakulima wa korosho na TADB itatoa dhamana asilimia 50 ya mkopo.
Alisema kuwa kutokana na TADB kuweka kipaumbele sekta ya kilimo itashirikiana na benki hiyo ili kuhakikisha kuwa mkulima wa korosho ananufaika na kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kumwondolea changamoto mbalimbali zinazomkabili.
“Gharama ya asilimia 50 itolewa na benki ya TADB ili kumwinua mkulima wa korosho katika msimu wa kilimo unaokuja ikiwa ni pamoja na kumwondolea kero mbalimbali alizokuwa anakabiliwa nazo ikiwa ni pamoja na kupata mkopo kwa urahisi,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Filbert Mponzi alisema kuwa NMB imetoa sh.Bilioni 9.5 kwa ajili ya kuwasaidia mikopo wakulima wa korosho kwenye mikoa inayolima zao hilo.
Alisema kuwa benki ya NMB inaweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo na ndio maana imekuwa ikimthamini mkulima kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu itakayomwezesha mkulima kupata pembejeo zote kwenye kilimo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo kutokana na kuwa na umuhimu mkubwa na ndio maana imekuwa imedhamiria kupitia upya sera na sheria ilim kumwezesha mkulima kunufaika na kilimo.
Bashe alisema kuwa benki nane zimeingia makubaliano ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo ambapo wakulima 2997 kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani wamenufaika na mikopo wa bili.9.5 iliyotolewa na NMB
Alisema kuwa katika kumwinua mkulima tayari benki nane ikiwemo NMB imejitokeza katika kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima ambapo Waziri Bashe ameziomba taasisi nyingine kujitokeza ili kumwinua mkulima ili kunufaika na kilimo.