Na Silvia Mchuruza,Kagera
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema ni vyema shughuli za uvuvi zikarasimishwa ili wavuvi waweze kunufaika kupitia sekta hiyo kwa kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha pamoja na kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Naibu Waziri Ulega amesema hayo Wilayani Muleba Mkoani Kagera wakati wa kikao na wawakilishi kutoka taasisi za kifedha, mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na baadhi ya wavuvi wa wilaya hiyo, ambapo amesema sekta ya uvuvi nchini zikiwemo shughuli zinazofanywa kwenye Ziwa Victoria bado hazijatoa mchango wa kutosha katika pato la taifa.
“Jumla ya thamani ya biashara ya mazao ya samaki kwa mwaka mmoja kwa Ziwa Victoria katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda inakadiriwa kuwa Shilingi Trilioni 6 wakati Tanzania inapata Shilingi Trilioni 1.6 wakati inamiliki eneo kubwa la ziwa ilhali Uganda na Kenya zinazomiliki eneo dogo zinapata Shilingi Trilioni 4.4 tafsiri yake ni kwamba bado hatujanufaika vya kutosha na Ziwa Victoria” Amesema Mhe. Ulega
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri Ulega ametaka shufghuli za uvu vi ziweze kurashimishwa na wavuvi waweze kupata mikopo ile kukuza sekta hiyo ambayo imekuwa ikitegemewa katika kuchangia pato la taifa na mtu mmoja mmoja.
Katika ziara hiyo pia Naibu Waziri Ulega ametembelea kijiji cha Mulela kilichopo Kata ya Kishanda na kutoa ahadi ya Shilingi Milioni Mbili kukarabati josho la kijiji hicho pamoja na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli ambaye amekuwa anakusanya mapato ili kumletea mwananchi maendeleo kwa kuboresha huduma mbalimbali za jamii.