Home Michezo SAMATTA AWEKA REKODI YAKE LIGI YA MABINGWA ULAYA (UEFA)

SAMATTA AWEKA REKODI YAKE LIGI YA MABINGWA ULAYA (UEFA)

0

*********************

NA EMMANUEL MBATILO

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ameweka rekodi mbili kwa mpigo, kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya,huku KRC Genk ikila kichapo cha Mbwamwitu cha magoli 6_2 na wenyeji, Red Bull Salzburg ya Austria Uwanja wa Red Bull Arena mjini Wals-Siezenheim.

Katika mchezo huo wa Kundi E, Samatta ambaye alikuwa anarejea uwanjani baada ya kukosekana kwenye mchezo wa Ligi ya Ubelgiji Ijumaa kufuatia kuumia akichezea timu yake ya taifa Stars jana alicheza kwa dakika zote 90 na kufunga bao lake dakika ya 52, wakati bao lingine la Genk lilifungwa na beki Mcolombia Jhon Janer Lucumi Bonilla dakika ya 40.

Mabao ya Red Bull Salzburg yalifungwa na mshambuliaji Mnorway mzaliwa wa England, Erling Haland dakika ya pili, 34 na 45, Mkorea Hwang Hee-Chan dakika ya 36, nyota wa Hungary, Dominik Szoboszlai dakika ya 45 na ushei na beki mkongwe wa Austria, Andreas Ulmer dakika ya 66.

Samatta msimu uliopita alikuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya UEFA Europa League na jana pia amejiwekea rekodi mbili mpya, kucheza Ligi ya Mabingwa, tena kuanza na kumaliza katika mechi ya kwanza na kufunga pia.

Jana Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26 amecheza mechi ya 163 kwenye mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.

Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 128 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Europa League mechi 24 katika mabao 14 na Ligi ya Mabingwa mechi moja, bao moja.