Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe akifafanua Jambao kwa Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani) Kuhusu Tamasha kubwa la Utamaduni kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) JAMAFEST 2019 litakalofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 21-28, 2019, Kulia ni katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiago Kilonzo, na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi (Habari na Picha) Kutoka Idara ya Habari-MAELEZO, Rodney Thadeus.
Mkurugenzi Msaidizi (Habari na Picha) Kutoka Idara ya Habari-MAELEZO, Rodney Thadeus, akiandika anachokisikia kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe wakatiwa Mkutano wa Waandishi wa Habari, Kuhusu Tamasha kubwa la Utamaduni kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) JAMAFEST 2019 litakalofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 21-28, 2019, Kulia ni katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiago Kilonzo.
………………….
Na. Dianarose Shirima-Maelezo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amezungumza na waandishi wa habari kuelezea uwepo wa tamasha la utamaduni la Afrika Mashariki JAMAFEST 2019 ambalo litafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 28 Septemba katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa maonyesho hayo yatajumuisha wasanii wanchi zote sita za Jumuiya ya Umoja wa Afrika Mashariki ambao ni wasanii wa ufundi kama vile wachonga vinyago, wachoraji, wabunifu wa mavazi, watengeneza bidhaa za vitenge, Batiki, wanasanaa wa ulimbwende, wasuka mikeka.
Vilevile wasanii wa taarabu, nyimbo za injili, wasanii wa maigizo, watungaji pamoja na wataalamu wa lugha ya Kiswahili na watafiti wa tiba za asili na vipodozi, hayo ndiyo makundi makubwa ambayo yatakuwepo siku hiyo pamoja na sanaa nyingine nyingi za ubunifu.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wasanii wa Muziki kama vile Peter Msechu ambaye ni mtunzi wa wimbo wa TANZANIA YA VIWANDA akiwa amewashirikisha wasanii wengine kama Mimi Mars, Linnah, Rich Mavoko ambao watakuwepo kwa ajili ya kuzindua wimbo huo, pia uwepo wa msanii mkubwa wa Tanzania anayepeperusha vyema bendera ya Tanzania Kimataifa Diamond Platnumz, “najua atakuwa na ziara yake Mkoani Iringa lakini nimemuomba kuahirisha kwa maslahi ya Taifa ni matumaini yangu atakubali kufanya hivyo”, alisema.
“Matamasha yaliyofanyika Rwanda, Kenya na Uganda miaka ya nyuma yalikuwa ni yenye Mafanikio makubwa ambapo wengi waliohudhuria walifaidika na maonyesho hayo, na kuendana kabisa na lengo la maonyesho hayo ambalo ni kuhifadhi, kulinda na kuendeleza urithi wa tamaduni za watu weusi wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla”, Alisema Dkt.Mwakyembe
Dkt. Mwakyembe amewahakikishia wahudhuriaji wote wa tamasha la JAMAFEST, Wanajumuiya wa nchi za Afrika Mashariki pamoja na watanzania kuwepo ulinzi na usalama katika tamasha hilo huku akitolea mfano wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokuja Jijini Arusha katika michezo kutoka nchi za Afrika Mashariki waliweza kukaa kwa muda wa siku kumi na waliondoka bila tatizo lolote hivyo hata katika maonyesho haya ya JAMAFEST yatakuwa ni yenye amani.
Mwakyembe amewataka watanzania kuwa wabunifu, licha ya yeye kutaja vitu vitakavyokuwepo katika maonyesho hayo amewataka watanzania kuwa na ladha tofauti kuwa ya hali ya juu ambayo itavutia watazamaji kutoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki, pia maonyesho haya yanahitaji ubunifu zaidi pamoja na kuonyesha vyakula vya asili ambavyo ni tamaduni ya watu weusi ‘vyakula vitapikwa vya aina mbalimbali lakini pia tutakuwa na madaktari ambao watathibitisha kwa afya za binadamu’ alisema.
Dkt. Mwakyembe amewakaribisha watanzania wote kuhudhuria maonyesho hayo kuonesha ubunifu wao na kufaidika na maonyesho hayo katika Nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Sambamba na hilo, Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amesema kuwepo kwa Tuzo ya filamu bora ambapo nchi zote za Afrika Mashariki wataleta filamu zao na kila nchi italeta filamu tatu ambapo ziashindanishwa ili kupata filamu tatu bora katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa upande wa Tanzania tayari wasanii wameshaanza kupeleka fiilamu zao na tayari wameshaambiwa ni filamu za aina gani zinazohitajika kwa ajili ya mashindano hayo, ‘nipende kuwakaribisha wasanii wote wa Tanzania kushiriki katika maonyesho hayo.