Sehemu wa wakuu wa Idara, taasisi na bodi za mazao wakifuatilia maelekezo ya kazi toka kwa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati wa kikao kazi katika ukumbi wa wizara jijini Dodoma leo.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (aliyesimama) akiongea wakati wa kikao kazi cha wizara na watendaji wakuu wa taasisi na wenyeviti wa bodi za mazao unaofanyika jijini Dodoma tarehe 17.09.2019 .Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Eng.Mathew Mtigumwe
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akitoa maelekezo ya kazi kuhusu uzalishaji na utafutaji masoko ya mazao nchini katika kikao kazi na Wakurugenzi,watendaji wakuu wa taasisi na bodi za mazao uliofanyika Dodoma tarehe 17.09.2019.
***********************************
Dodoma
Watendaji wa wizara ya kilimo na taasisi zake wameagizwa kufanya kazi
kwa weledi na maarifa ili kuweza kufikia malengo ya uzalishaji mazao
nchini.
Agizo hili limetolewa leo (17.09.2019) jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo
Japhet Hasunga wakati wa kikao kazi cha watendaji wa wizara ,taasisi na
bodi za mazao kujadili taarifa za utekelezaji wa malengo ya mwaka
2018/2019.
Waziri Hasunga amewajulisha watendaji hao kuwa bado wizara na taasisi
zake hazijafanikiwa kufikia lengo ya uzalishaji wenye kuzingatia tija na
kuwezesha kilimo kiwe cha kibiashara.
“Takwimu zinaonyesha hatujafanya vizuri kwenye kusaidia upatikanaji wa
masoko ya mazao ya wakulima nchini kwa kipindi cha mwaka 2018/2019”
Waziri Hasunga alieleza.
Aliongeza jukumu la wizara ni kuhamasisha uzalishaji na kuhakikisha
mazao ya wakulima yanaongezwa thamani ili kuwa na soko la uhakika
Waziri Hasunga alisema changamoto ya masoko kwa mazao ya wakulima
inahitaji kuwekewa mfumo mahsusi wa utatuzi ,hivyo ni jukumu la
wataalam kuja na mipango mizuri ya utekelezaji.
‘Wizara yetu inasimamia aina 85 za mazao nchini “ hii inafanya wizara
kuhitaji weledi na utaalamu kupata ufumbuzi wa haraka wa changamoto
za mazao haya, alisisitiza Waziri Hasunga.
Waziri wa kilimo ametaja malengo sita (6) ambayo serikali ya awamu ya
tano inatumia kupima utendaji kazi wa wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020,
kwanza ni kuhakikisha nchi inazalisha chakula cha kutosha na kuwa na
usalama wa chakula.
Pili,kilimo kinachangia upatikanaji wa fedha za kigeni, na tatu kilimo
kinatoa mchango mkubwa katika pato la taifa zaidi ya asilimia 30 ya sasa.
Kigezo cha nne ni malighafi kiasi gani inapatikana kwa matumizi ya
viwandani,tano kiasi gani cha ajira zimezalishwa katika sekta ya kilimo na
sita namna gani wizara inasimamia ushirika nchini kuwa na tija na kuondoa
kero.
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewapongeza watendaji wote
waliopo chini ya wizara hiyo kwa utendaji mzuri uliofanikisha Tanzania
kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kati ya nchi za Afrika
Mashariki mwaka 2019.
“Nawapongeza wote waliosaidia nchi yetu kuzalisha mahindi kwa asilimia
103 na kuongoza Afrika Mashariki hali iliyofanya nchi kuwa una utoshelevu
wa chakula wa asilimia 119” alipongeza Waziri Hasunga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini Marco
Mtunga ameelezea mafanikio ya zao hilo kuwa hadi kufikia mwezi huu
Septemba tani 301,132 za pamba zimekusanywa toka kwa wakulima
ikilinganishwa na tani 222,039 mwaka 2018.
Ameongeza kusema kuwa bodi imefanikiwa kusambaza chupa milioni sita
za viuatilifu kwa wakulima katika msimu huu 2019/2020 ili kudhibiti
magonjwa kwenye zao hili.
Hata hivyo,Mtunga ameeleza kuwa zao la pamba linakabiliwa na
changamoto kubwa ya soko kutokana na ukosefu wa wanunuzi wa
uhakika.
“Tunaiomba serikali iingilie kati suala la upatikanaji wa soko la uhakika la
pamba hususani katika mkoa wa Katavi ambako mvua sasa imeanza
kunyesha na wakulima bado hawajauza pamba yao” alisema Mtunga
Katika hatua nyingine,Mwenyekiti wa Bodi ya Nafaka na Mazao.
Mchanganyiko Monica Mbega amesema bodi imefanikiwa mwaka huu
kuanza kuzalisha unga wa mahindi tani 180 kwa siku katika viwanda vya Arusha (60),Iringa (60) na Dodoma(60) zinazokidhi viwango vya soko la kimataifa.