KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, Mwenyekiti wa Bodi ya UTT Amis Bw. Casmir Kyuki , Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)Bw. Nicodemus Mkama wakizindua Mfuko wa Uwekezaji wa Hatifungani (BOND Fund) wa kampuni ya UTT Amis katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)Bw. Nicodemus Mkama mara baada ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Hatifungani (BOND Fund) wa kampuni ya UTT Amis katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. wa pili kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala na Mwenyekiti wa Bodi ya UTT Amis Bw. Casmir Kyuki.
………………………………………………….
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amezindua mfuko mpya wa uwekezaji wa pamoja ujulikanao kama Mfuko wa Hatifungani (Bond Fund) unaomilikiwa na Kampuni ya UTT-AMIS, wenye lengo la kuwawezesha wawekezaji wadogo na wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi kuweka akiba, kukuza mitaji na kipato chao.
Akizindua Mfuko huo Jijini Dar es Salaam, Bw. James ameiagiza Kampuni ya UTT-AMIS kutoa elimu ya kutosha kwa umma ili wananchi wengi zaidi wanufaike na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili kuwawezesha kumiliki uchumi wa chi yao.
Alisema kuwa UTT-AMIS inamiliki mifuko mitano yenye thamani ya sh. bilioni 300 ikiwa na wawekezaji 145,000 pekee ikilinganishwa na idadi kubwa ya watanzania.
“Namba hii ni ndogo na jitihada kubwa inahitajika ili kuwafikia watu wengi zaidi, hivyo nawaelekeza muendelee kutoa elimu kwa wananchi na wadau wengine wote ili mifuko hii iwe chachu ya maendeleo nchini” alisema Bw. James
Alitoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali kuchangamkia fursa za kuwekeza katika Mfuko huo mpya wa Hatifungani kwa kuwa ni salama na una faida kubwa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala, alisema kuwa mwekezaji anaweza kuwekeza kwenye Mfuko huo mpya kuanzia sh. 50,000.
“Mwekezaji atakaye wekeza sh. 10,000,000 atapata gawio kila mwezi, atakaye wekeza sh. 5,000,000 atapata gawio la mara moja kila baada ya miezi sita wakati watakaowekeza sh. 50,000 na zaidi watapata fursa ya kukuza mitaji yao” alisisitiza Bw. Migangala
Alifafanua kuwa Bond Fund ni uwekezaji wa pamoja uliowazi ambao utawekeza kwenye hatifungani za Serikali, hatifungani za mashirika na uwekezaji katika masoko ya fedha lengo kuu likiwa ni kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika soko la mitaji
UTT-AMIS inasimamia na kuendesha mifuko mingine mitano ikiwemo Mfuko wa Umoja, Mfuko wa Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu na Mfuko wa Ukwasi.