Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kabla ya kuzindua mfumo wa Rada za kuongozea Ndege katika kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
*************************************
Na Paschal Dotto
MAELEZO
DAR ES SALAAM
16.9.2019
RAIS Dkt. John Magufuli amewataka watendaji wanaosimamia miradi ya Serikali kutumia vifaa vinavyozalishwa na viwanda vya ndani ili kuinua sekta ya viwanda na kuongeza ajira kwa watanzania wanaofanya kazi katika viwanda hivyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza mabomba ya plastiki cha Pipe Industirial Co.Ltdleo (Septemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa Serikali inatekeleza miradi mingi mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na sekta ya umwagiliaji ambayo yote hiyo inatumia mabomba ya kusafarisha maji.
“Miradi yote inayotekelezwa na Serikali inahitaji matumizi ya mabomba kwa asilimia 100, kwa hiyo ni lazima tutumie mabomba yanayotengenezwa nchini, sijasema tusiagize pengine lakini lazima tuwe wazalendo ili kuinua sekta yetu ya viwanda kwa kulinda viwanda vyetu vya vinavyozalisha bidhaa mbalimbali hapa nchini” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuwa viwanda vinavyojengwa nchini vitakuwa na faida nyinyi kwa wananchi na kwa Serikali kwa ujumla ikiwemo, upatikanaji wa ajira, ambapo Serikali itakusanya kodi ambazo zitatumika katika ujenzi wa barabara, ununuzi wa Ndege, ununuzi wa madawa, pamoja na uuzaji wa bidhaa zinazoenda nje zitakazoifanya Serikali kupata fedha za kigeni.
AIdha Rais Magufuli alisema katika kuhakikisha sekta ya Viwanda imekua, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufufua viwanda vuilivyokufa, kuondoa urasmu katika taasisi zinazohusika na viwanda kama TBS, TFDA, NEMC, OSHA na Taasisi zinginezo ili kuwawezesha wawekezaji kuja kuwekeza kwa wingi nchini.
“Serikali imefanya yote hayo kwenye Taasisi husika, lakini pia imeweza kupunguza utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara na kwa wenye viwanda, kwa mwaka huu wa fedha tumefuta tozo zipatazo 54 ambazo zingekuwa zinakwamisha juhudi za Serikali za kuwa na viwanda vya kutosha”, Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa kiwanda cha Pipe Industirial Co.Ltd Jijini Dar es Salaam ni kiwanda ambacho kinatumia teknolojia ya kisasa kuzalisha mabomba ambapo uwekezaji wake umetumia Bilioni 120 kwa wawekezaji kujenga kiwanda hicho.
“Nimefurahi kusikia kwamba wakati wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanda hiki watu wapatao 215 wamepata ajira, ambapo awamu ya pili itakapokamilika kiwanda hiki kitaweza kuzalisha mabomba ya kusafirisha gesi, mafuta na nyaya za umeme na kitaajili watu wapatao 500 hii ni hatua kubwa katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati wenye viwanda”, Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli, alisema kuwa Sekta ya viwanda ni Sekta muhimu kwa nchi yoyote duniani, kwani Takwimu za Shirika la Biashara Duniani (WTO) zinaeleza kuwa asilimia 70 ya biashara ya kimataifa kwa mwaka 2018 bidhaa za viwandani zilichukua nafasi kubwa na kuwa na thamani ya dola za kimarekani Trilioni 12.41 ikifuatiwa na bidhaa ya mafuta asilimia 15, bidhaa za kilimo asilimia 10 na bidhaa nyinginezo asilimia 5 na thamani yake ni dola trilioni 5.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa, alisema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo inalenga kuwasaidia wafanyabiashara kuzalisha kwa kulenga masoko yote ndani na nje ya nchi ili kuinua sekta hiyo muhimu nchini.
“Kiu ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni kuona Tanzania hatuzalishi tu kwa soko la ndani, bali tunazalisha kwa ajili ya masoko ambayo Tanzania ni mwanachama wa jumuiya mbalimbali, kwa hiyo uzalishaji katika viwanda vyetu ni vizuri ukalenga masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika(SADC) na Soko la Pamoja la Nchi Huru za Afrika (AU)”, Waziri Bashungwa.