Na Silvia Mchuruza, Kagera;
Wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) Mkoani Kagera wametakiwa kuacha mara moja vitendo vya kuwaruhusu watoto wao kuchunga mifugo wakati wa jua Ili kuepuka ugonjwa wa saratani ya ngozi utokanao na mionzi ya jua.
Ushauri huo umetolewa leo Septemba 16, 2019 na Daktari wa magonjwa ya ngozi kutoka mkoani Mara Lucas Simba wakati akitoa elimu kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ualbino katika kliniki maalumu iliyofanyika katika Hospitali ya mkoa iliyopo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Elimu hiyo imetolewa wakati shirika lisilo la kiserikali la Standing Voice Tanzania kutoka jijini Mwanza likikabidhi vifaa kwa watu wenye ualbino ikiwemo kofia pana kwa watoto kuanzia umri wa miaka 0-2, mafuta maalum kwa ajili ya ngozi na miamvuli kwa ajili ya watoto wachanga.
Simba amesema kumekuwepo kwa baadhi ya wazazi na walezi ambao wamekuwa na tabia ya kuwaruhusu watoto wao kwenda kuchunga mifugo wakati wa jua ambapo hukutana na changamoto mbalimbali ikiwemo mionzi ya jua inayosababisha ugonjwa wa saratani ya ngozi.
Amesema wazazi wanapaswa kubadilika ili kuokoa maisha ya watoto wao na kuwa mtu mwenye ualbino asiyejikinga na jua atapata madhara makubwa ikiwemo kuwa na wekundu wa ngozi, kutokwa vidonda mdomoni na usoni, maumivu mwili mzima jambo linalosababisha kupata saratani ya ngozi.
Amewataka wazazi hao kuwakinga watoto wao dhidi ya jua kwa kuwavalisha kofia pana ,kuwapaka mafuta maalum, kukaa kivulini, kutumia miamvuli.
Naye Mratibu wa huduma za afya kutoka shirika la Standing Voice Tanzania la jijini Mwanza Kaballa Maganja amesema wazazi wanapaswa kuwajibika vyema kwa watoto wao katika kujikinga na madhara ya jua kwa kuvitumia vyema kofia pana,mafuta na miamvuli.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha watu wenye ualbino mkoa wa Kagera Burchard Mpaka ametaja changamoto ya kejeli na unyanyapaa katika jamii kwani baadhi ya watu huwaita majina ya ajabu.
Mama mwenye ualbino Anitha Lyimo kutoka wilayani Misenyi mkoani hapa ametajwa kukerwa na baadhi ya akina mama wanaokuwa wanawapeleka watoto wao wenye ualbino kliniki kwa kuwaficha na kuwashauri kuacha tabia hiyo badala yake watimize masharti ili waendelee kuishi kwa amani.