Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Kushoto) akikabidhi cheti cha kuthamini mchango wa USAID kwa Mkurugenzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (Ps3) Dr. Emmanuel Malangalila (Kwanza kulia) pamoja na Germin Mtei
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Kushoto) akikabidhi cheti cha kuthamini mchango wa PS3 kwa Mkurugenzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (Ps3) Dr. Emmanuel Malangalila (Pili kulia).
Mkurugenzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) katika kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani).
Mkurugenzi wa TEHAMA OR-TAMISEMI Erick Kitali akiwa na Germin Mtei kutoka Ps3 katika kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani).
Kaimu Katibu Mkuu 0R-TAMISEMI Beatrice Kimoleta akizungumza katika kiao alichokiitisha Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI pamoja na viongozi wa Mradi wa Ps3.
……………………………
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo (Mb) amepongeza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma (Ps3) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo imepelekea uboreshaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia OR-TAMISEMI.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kikao maalum na Uongozi wa Mradi huo kilichofanyika Ofisini kwake Mtaa wa Tamisemi, Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo alisema Ps3 mmetuweka katika nafasi nzuri sana haswa katika eneo la Miundombinu ya TEHAMA, mmefanya kazi kubwa katika kila eneo linalohitaji mifumo, mmewajengea uwezo watumishi wetu hakika najivunia sana Ps3 sababu mmeifanya kazi yetu imekua rahisi sasa kupitia mifumo hii.
Zaidi mmekuwa na ushirikino mkubwa sana kila tunapohitaji, mahusiano kati ya TAMISEMI na Ps3 yamekua na kuimarika vya kutosha mmekuwa watu wema, wasikivu na watekelezaji kupitia uongozi wenu makini tumebadili vitu vingi sana kupitia Mradi wa Ps3 alisisitiza Mhe. Jafo.
“Nimeona leo niwaite rasmi kuwapongeza na kuwashukuru kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya najua tumekutana mara kwa mara kwenye kazi mbalimbali lakini leo nimeamua iwe maalumu nikutane na Uongozi niweze kuongea haya ambayo kila wakati nimekuwa nikitamani kuyafikisha kwenu” Aliongeza Jafo.
Jafo aliongeza kuwa Shukrani zangu haziwezi kuja mikono mitupu nitawakabidhi vyeti vya kuthamini mchango wenu mlioutoa katika Ofisi yangu: Cheti kimoja ni kwa ajili ya Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ambao ndio wamekua wakitoa Fedha na cheti kingine ni kwa ajili yenu Ps3 ambao mmekua watekelezaji wa kazi za mradi huu.
“OR-TAMISEMI inajivunia kushirikiana na Ps3 katika kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi, kazi mnayoifanya imewezesha kuwa na Serikali yenye uwazi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja” alimalizia Jafo.
Mkurugenzi wa Mradi wa Ps3 Dr. Emmanuel Malangalila ameishukuru Serikali kwa ushirikiano walioupata wakati wote wa utekelezaji wa kazi za mradi wa Ps3.
“Tumefanya kazi katika Sekta mbalimbali na kazi zetu zimegusa maeneo ya Elimu, Afya, Fedha na hata mpaka kwenye Kilimo na kote huko tumepata ushirikiano ambao ulifanya kazi za mrdai huu kuwa nyepesi na kutekelezeka kwa urahis” Alisema Dr. Malangalila.
Dr. Malangalila aliongeza kuwa Mradi huu unatekelezwa katika Mikoa 13 Tanzania bara lakini kazi tulizozifanya zimegusa mikoa yote 26 hii imetokana na uhitaji na umuhimu wa kazi za mradi katika kila Mkoa.
Tumefurahi leo Waziri Jafo kutambua mchango wa Ps3 na tunaahidi kuendelea kuboresha kila eneo ambalo tumelifanyia kazi na tunaona bado kuna umuhimu wa kuimarisha zaidi alimalizia Dr. Malangalila.
Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ulioko chini cha USAID unafanya kazi katika mikoa 13 na Halmashauri 93 Tanzania Bara ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za umma kwa njia ya utawala bora, fedha, rasilimali watu, na mifumo ya taarifa.