Mbaga: Mfuko wa Hati Fungani kutoa fursa kwa jamii kujikomboa kiuchumi

  0

  Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi
  Mbaga, akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani)

  **********************

  Na Mwandishi Wetu

  KAMPUNI ya UTT AMIS inayomilikiwa na Serikali kupitia
  Wizara ya Fedha na Mipango, imeanzisha huduma mpya ya
  Mfuko wa Hati Fungani ‘Bond Fund’ ili kuiwezesha jamii iweze
  kuzifikia fursa za uwekezaji na kujikomboa kiuchumi.

  Kuanzishwa kwa mfuko huo kumeongeza idadi ya mifuko na
  kufikia sita yote ikisimamiwa na kampuni hiyo iliyoanzishwa
  mwaka 2013 ikichukua jukumu ya usimamizi wa Mifuko ya
  Uwekezaji wa Pamoja kutoka kwa Dhamana ya Uwekezaji
  Tanzania (UTT).

  Akiuzungumzia mfuko huo, Mkurugenzi wa Masoko na
  Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, alisema utatoa fursa
  kwa wawekezaji wadogo, wakati kuzifikia fursa za uwekezaji
  zilizokuwa zikifikiwa na wawekezaji wachache, wakubwa.

  Alifafanua kuwa, baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka kirahisi
  ambapo namna ya kuzifikia, kuwekeza ni rahisi lakini wakati
  mwingine hazitoi faida shindani kwa wawekezaji.

  Alisema mfuko huo utaondoa changamoto ambazo huwakuta
  wawekezaji kwenye soko la fedha ambalo lina bidhaa nyingi
  zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji.

  “Mbali ya Mfuko wa Hati Fungani, UTT AMIS inasimamia
  mifuko mingine ya uwekezajiambayo ni Mfuko wa Umoja,
  Wekeza Maisha, Watoto, Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi.

  “Kuanzishwa kwa Mfuko wa Hati Fungani kumetokana na
  mahitaji ya wawekezaji pamoja na uchambuzi wa bidhaa za
  kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa,” alisema.

  Mbaga alisema mfuko huo utawekeza kwenye hati fungani
  zilizoorodheshwa katika soko la hisa kwa asilimia 90, asilimia
  10 itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.

  Lengo ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha
  kutokana na uwekezaji wao waweze kufanya hivyo, kumfanya
  mwekezaji achague kama anapenda kukuza mtaji au kupokea
  gawio kila mwezi, kila miezi sita kulingana na hitaji lake.

  Alisema kampuni hiyo pia inatoa huduma ya usimamizi wa mali
  za kifedha ili kukidhi mahitaji maalum kwa wawekezaji binafsi
  wa kipato cha kati, cha juu na taasisi.

  Aliongeza kuwa, baadhi ya wawekezaji hasa wadogo ni vigumu
  kuwekeza katika baadhi ya bidhaa kwenye soko la fedha, Mfuko
  wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa changamoto hizo.

  “Mwekezaji anapata faida sawa na wawekezaji wakubwa,
  akihitaji fedha anauza baadhi ya umiliki wake kwenye mfuko
  kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.

  “Mfuko pia unawafaa wawekezaji wakubwa kwani ina faida
  shindani, gharama ndogo za kuwekeza, ukwasi wa kutosha,
  usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji,” alifafanua.

  Alisema mfuko huo hutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza,
  kushiriki katika masoko ya mitaji, kufaidika na uwekezaji huo,
  umeanzishwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kipato cha
  chini, kati na kipato cha juu.

  Mbaga alisema watu binafsi, kampuni, taasisi, vikundi rasmi
  wanaweza kushiriki katika uwekezaji kwenye mfuko huo, lengo
  ni kuwafanya wawekezaji wawe na ushiriki mpana kupitia
  uwekezaji wa vipande, kuhamasisha utamaduni wa kuweka
  akiba kupitia hati fungani na masoko ya fedha.

  Mfuko huo unatoa fursa ya uwekezaji rahisi wa muda mrefu
  kwa wawekezaji wanaopenda kuwekeza ili kukuza mtaji, kupata
  gawio kila mwezi au baada ya miezi sita kama anavyohitaji.

  “Kimsingi Mfuko wa Hati Fungani una mipango miwili ya
  uwekezaji ili kukidhi matakwa tofauti ya wawekezaji, kuna
  mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio kila baada
  ya miezi sita.

  “Mpango wa kukuza mtaji, gawio la mara kwa mara
  halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana
  itarudishwa kwenye uwekezaji wa awali kwa kununua vipande
  vitakavyonunuliwa kwa bei ya wakati huo.

  “Mpango huo utawafaa wawekezaji wanaohitaji kuweka akiba
  kwa malengo maalum mfano kujenga nyumba au wafanyakazi
  wenye kipato na wangependa kuwa na fedha ya akiba kama
  dharura itatokea au kwa matumizi ya baadae wanaweza
  kuchagua mpango wa kukuza mtaji,” alisema.

  Mbaga alifafanua kuwa, wawekezaji katika mpango huo
  wanaweza kuuza kiasi chochote cha uwekezaji kama watakidhi
  vigezo ya mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande.

  Mpango wa gawio kila mwezi hutokana na mahitaji ya kifedha
  ya mwekezaji na anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya
  kuwekeza kwenye mfuko.

  Wawekezaji ambao wanahitaji kuchukua faida kila mwezi
  mfano wastaafu wanaopata fedha zao za mkupuo, kuwekeza
  kwenye mfuko wanashauriwa kupokea gawio kila mwezi ili
  wapate kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata.

  Mbaga alisema wawekezaji wengine wanaopata fedha nyingi
  kwa mara moja mfano wachimba madini wadogo, wanaweza
  kuchagua kupata gawio kila mwezi ili waweze kuendesha
  shughuli zao bila kuathiri mtaji walioupata.

  Pia wawekezaji watakaojiunga na mpango huo wanaweza kuuza
  vipande kidogo au vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya
  mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande vya mfuko.

  Wawekezaji wanaopata fedha nyingi kwa msimu kama
  wakulima wa mazao mbalimbali, wanaweza kuchagua gawio la kila miezi sita ili waweze kupata fedha wakati wa kuandaa mashamba yao, kulima na kuvuna ili waweze kuendesha
  shughuli zao, kufuata msimu bila kupoteza mtaji.

  Akizungumzia gharama za kuwekeza, Mbaga alisema hakuna
  gharama yeyote wakati wa kujiunga au kujitoa kwenye Mfuko
  wa Hati Funganui, wawekezaji wataruhusiwa kununua, kuuza
  vipande kwa thamani halisi ya kipande itakayokuwepo.

  “Wawekezaji wote wa ndani na nje ya Tanzania kama Sheria ya
  Soko la Mitaji na Dhamana inavyoruhusu, wanaweza kuwekeza
  kwenye mfuko huu,” alifafanua.

  Kuhusu ununuzi wa vipande, alisema vinaweza kununuliwa siku
  yoyote ya kazi isipokuwa kipindi cha kufunga vitabu ambacho
  hakitazidi siku saba za kazi.

  Alisema kuanzia Septemba 16, mwaka huu hadi Oktoba 16,
  mwaka huu, itakuwa kipindi cha mauzo ya awali hivyo ni vizuri
  Watanzania wakachangamkia fursa hiyo.

  Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na thamani halisi ya
  kipande itakuwa sh. 100 ambapo maombi ya kununua vipande
  yanaweza kuwakilishwa katika tawi lolote la Benki ya CRDB;
  ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es
  Salaam; Ofisi za Shirika la Posta au Wakala yoyote
  atakayeteuliwa na UTT AMIS.

  “Uwekezaji katika mfuko huu kwa wawekezaji walio nje ya
  Tanzania, awasiliane na ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au ofisi za UTT AMIS ili kupata taarifa na muongozo zaidi.

  Anaongeza kuwa, thamani ya mwanzo ya kipande itakuwa sh.
  100. Thamani ya kuuza na kununua kipande itakuwa sawa na
  thamani halisi ya kipande bila gharama yoyote.

  Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na hakuna ukomo
  kwenye kiwango cha juu, hiyo ni fursa kwa kila Mtanzania
  ambapo baada ya muda wa mauzo ya awali, mwekezaji anaweza
  kuwekeza kuanzia sh. 5000, mara nyingi kadri awezavyo.

  Malipo ya mauzo ya vipande yanaweza kufanywa kwa fedha
  taslimu au hundi ya benki itakayolipwa kwenye akaunti ya
  Mfuko wa Hati Fungani iliyopo Benki ya CRDB.

  “Wawekezaji wanaweza kwenda kwenye tawi lolote la Benki ya
  CRDB na kufanya malipo. Pia malipo yanaweza kufanyika kwa
  kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money,” alisema.

  Mbaga alisema kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa
  mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa Kukuza Mtaji ni vipande
  500. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100,
  thamani ya chini ya vipande, mauzo itakuwa sh. 50,000.

  Kuhusu mpango wa gawio kila mwezi, kiwango cha chini cha
  uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa mpango wa gawio
  kila mwezi ni vipande 100,000, thamani ya mwanzo ya kipande
  sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh.
  10,000,000.

  Mpango wa gawio kila miezi sita, kiwango cha chini cha
  uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa gawio
  kila miezi sita ni vipande 50,000, thamani ya mwanzo kwa
  kipande sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo
  itakuwa sh. 5,000,000.

  Alitoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi
  akiwahimiza wawe sehemu ya uwekezaji katika mfuko huo
  mpya kwani una faida nyingi, hawapaswi kuwa na hofu.