Katibu wa Sheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Elias Mwashiuya (kushoto), akilishwa keki na watumishi waliostaafu wa
Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), katika hafla ya kuwaaga baada ya kustaafu hivi
karibuni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, akiongea na watumishi walioudhuria hafla
ya kuwaaga watumishi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), waliostaafu hivi karibuni jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Paul Rwegasha akimkabidhi mmoja wa Watumishi waliostaafu wa Idara
ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa JNIA, Mhandisi Bertha Kipenda zawadi ya
vifaa vya mazoezi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es
Salaam.
Kaimu Meneja wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Diana
Munubi (kushoto), akimkabidhi zawadi picha ya ua Ernest Kevela (wa kwanza
kulia) katika hafla ya kuwaaga wastaafu wa Idara hiyo iliyofanyika hivi karibuni
Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (kushoto), akimkabidhi zawadi ya ngao,
Theobald Benigius wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi katika Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) katika sherehe ya kuwaaga
Wastaafu baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria na taratibu za Utumishi wa
Umma.
Watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiserebuka kwa kucheza muziki katika
hafla ya kuwaaga watumishi wenzao wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi
waliostaafu hivi karibuni.
*******************
Na Bahati Mollel, TAA JUHUDI, maarifa na upendo ndio vigezo vitatu vilivyotajwa
na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania, (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama kuwa ni
chachu ya kuipandisha hadhi taasisi hiyo.
Mhandisi Ndyamukama ametoa rai hiyo juzi katika
sherehe ya kuwaaga Watumishi waliostaafu kwa mujibu
wa sheria wa Utumishi wa Umma wa Idara ya Uhandisi na
Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa hadhi ya taasisi hiyo imeshuka mbele
ya uso wa nchi na jamii na kusababisha baadhi ya kazi
ilizokuwa ikizifanya zamani, sasa kupewa taasisi nyingine.
“Nashauri tupendane na tuchape kazi kwa bidii, kwani
sura yetu kama TAA hapo katikati imedorora, kwani
tumepoteza kazi nyingi, hivyo tukitaka kurudisha hadhi
yetu itahusu kusukumana, nitaomba mnivumilie, lakini
lengo likiwa ni kutaka kurudisha TAA ya zamani ingawa
najua wapo, ambao hawataki hivyo,” amesema Mhandisi
huyo.
Hatahivyo, amewashukuru watumishi wenzake kwa
kumpokea vizuri tangu kuteuliwa kwake kuongoza taasisi
hiyo, takribani miezi sita iliyopita, ambapo amekiri
kubobea zaidi katika masuala ya ujenzi wa barabara,
lakini sasa kwa muda mfupi aliokaa ameweza kwenda
sambamba na wataalam wa viwanja vya ndege kwa
kujifunza masuala yote muhimu ya viwanja hivyo.
“Wengi wamenisaidia kuelewa hii kazi, kwani nilikuwa
nikitegemea Watumishi wote waniongoze na kunifundisha,
na sasa naelewa kazi za aviation, ila la msingi nasisitiza
hapa tupendane na tuchape kazi kama wenzetu
wanaostafu leo (juzi) kwa mujibu wa taratibu na sheria za
utumishi wa umma,” amesema.
Pia ameweka angalizo kwa Watumishi wote kuwa muda
wote atakaokuwepo hapo kama Mkurugenzi Mkuu,
atalazimika kuwasumbua na kuwasukuma, ili sura ya TAA
ambayo hapo katikati imedorora kwa kupoteza kazi
nyingine mbele ya wananchi na taifa, ing’are tena.
Akiwapongeza wastaafu hao amewataka kuendelea
kufanya kazi wawapo majumbani mwao, ili kuimarisha
afya ya mwili na akili.
“Ninawapongeza sana Wastaafu wote bado mna nguvu ya
kufanyakazi pamoja na kustaafu, muwe mnapitapita
sehemu mbalimbali kuendelea na kazi zenu maana
mmestaafu, lakini hamjachoka, bado ‘you’re retired but not tired’” pia nawapongeza sana walioandaa shughuli hii, ambayo imefana sana”, amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha
amesema watumishi hao walikuwa na nidhamu kubwa na
kufanya kazi kwa bidii, pasipo kuchoka wala kuwa na
malalamiko, ambapo amewataka watumishi wengine
kuiga mfano huo uliotukuka.
Lakini, pia amewataka Wastaafu hao kuendelea kufanya
mazoezi, kwani wamekuwa wakifanya kazi ngumu
wawapo katika kituo chao cha kazi cha JNIA.
“Wote nikiwaangalia mlikuwa mkifanyakazi kwa bidii hadi
usiku mwingi, hivyo mnahitajika kuendelea kufanya
mazoezi ya viungo asubuhi na jioni na mkifanya hivi
mtafikisha ule umri wa ahadi wa miaka 120 (Mwanzo sura
ya 6), ile mingine ya miaka 80 ni ya Mfalme Daudi ila hii
120 ni ya Mwenyezi Mungu mwenyewe, mlikuwa mkiwahi
shuttle kuwahi kazini lakini sasa muamke na kufanya
mazoezi,” amesema.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na
Huduma za Ufundi, Mhandisi, Alex Kalumbete amesema
wastaafu hao walikuwa na uvumilivu mkubwa katika
utumishi wa umma kutokana na kazi ngumu walizokuwa
wakifanya za kiuhandisi.
Kaimu Meneja Uhandisi na Huduma ya Ufundi JNIA,
Diana Munubi amesisitiza upendo uendelee kuwepo baina ya watumishi kama vile wastaafu hao walivyokuwa wakiuenzi wakati wa utumishi wao wote wa umma.
Mmoja wa wastaafu hao, Bw. Theobald Benigius kwa
niaba ya wenzake ameishukuru TAA kwa kuwezesha
kufanya kazi vizuri hadi utumishi wao kukoma kwa
kustaafu, na amewaomba watumishi wenzake kuwa
wavumilivu na tabia njema, kwani wataweza kustaafu
vizuri.