Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za fedha ya mwaka 2018 haina lengo la kuinyima jamii fursa ya kusaidiana kwa njia ya kukopeshana bali inalenga kutatua changamoto zilizopo ikiwemo ya utozaji wa riba kubwa.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Lucy Magereli, aliyetaka kujua Sheria ya udhibiti wa taasisi ndogo za fedha imetekelezwa kwa kiasi gani na Serikali haioni Sheria hiyo inainyima jamii kusaidiana.
Dkt. Kijaji alisema kuwa kutokana na changamoto za Sekta ndogo ya Fedha ikiwemo kutoza kiwango kikubwa cha riba na ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda walaji na wadau kwa ujumla, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 itaimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo.
“Udhibiti wa sekta ndogo ya fedha unaakisi matarajio na mahitaji ya wadau na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji na mchango wake katika sekta nzima ya fedha na uchumi kwa ujumla”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa walengwa wa Sheria hiyo wamepewa mwaka mmoja wa mpito baada ya kanuni kutolewa ili waweze kujiandaa kulinganana matakwa ya kanuni hizo ambazo zitaanza kutumika rasmi baada ya kipindi hicho kupita.
Dkt. Kijaji alisema kuwa hadi sasa hakuna taasisi yoyote iliyosajiliwa kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.
Alifafanua kuwa, baada ya Sheria hiyo kutungwa, Serikali ilianza mchakato wa kuandaa kanuni za huduma hiyo zilizolenga madaraja manne ya watoa huduma yaliyoainishwa kwenye Sheria.
Mchakato huo ulihusisha ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za walengwa ili kuweza kutengeneza kanuni zilizozingatia hali halisi ya biashara zao pamoja na matakwa ya Sheria. Aidha mchakato wa kuandaa kanuni ulikamilika na hivyo kutangazwa kwenye gazeti la Serikali namba 575 Agosti 2, 2019.