Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) inatekeleza mradi wa Tanzania Urban Resilience Programme (TURP) ambao umelenga kuzisaidia Halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mh. George Simbachawene alipokua akijibu swali la Mbunge wa Temeke Mh. Ally Mtulia lililouliza Je ni lini Serikali itajenga Mto Msimbazi?.
Waziri Simbachawene aliongeza kuwa Mradi huu ukitekelezwa utaleta manufaa makubwa katika Jiji la Dar es Salaam ambapo utaokoa maeneo yaliyo hatari kwa mafuriko na kuyafanya salama kwa maendeleo ya jiji, utapendezesha jiji kwa kuweka maeneo mazuri ya maegesho ya magari (Dar Central Park, First of its Kind in Tanzania and East Africa), maeneo kwa ajili ya shughuli za umma kama mikutano na matamasha na kubadilisha eneo la Mto Msimbazi linalokumbwa na mafuriko kuwa eneo linalofaa kwa ajili ya michezo na lenye manufaa ya kiikolojia kwa jiji la Dar es Salaam.
Naye Mbunge wa Jimbo la Wingwi kutoka Zanziba Mh. Juma Kombo Wawi, aliuliza Je, Serikali haioni ni busara kuondoa suala la uvuvi wa Bahari kuu kwenye orodha ya mambo ya Muungano ili kuisaidia Zanzibar kujiendesha yenyewe na kuweza kusaidia uchumi wa Zanzibar.
Akijibu swali Hilo Waziri Simbachawene alisema kuwa Bunge lilipitisha Sheria ya Territorial Sea and Exclusive Economic Zone Act, 1989 iliyoanzisha Maeneo ya Bahari yaitwayo Bahari ya Ndani (Inner Sea), Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) na Eneo la Uchumi la Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ). Chimbuko la Sheria hii ni Sheria ya Kimataifa ya Bahari (The United Nations Convention on the Law of the Sea (UNCLOS), ya Mwaka 1982 inayotoa fursa sawa kwa nchi duniani kugawana rasilimali za bahari zilizopo kwenye maji (water column) na pia kwenye sakafu ya bahari (seabed).
Mheshimiwa Spika, Tanzania iliridhia na kuanza kuitekeleza Sheria hii mwaka 1985. Hivyo, jukumu la kusimamia shughuli za uvuvi kwenye maji yaliyo katika Bahari ya Ndani (Inner Sea) na Bahari ya Kitaifa (Territorial Sea) ya Tanzania Bara hutekelezwa kupitia Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003, na upande wa Zanzibar Sheria ya Uvuvi Na. 7 ya Mwaka 2010. Ili kutekeleza Sheria ya mwaka 1989 hususan katika kusimamia rasilimali za uvuvi zilizopo kwenye eneo la ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania (EEZ) lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zilikubaliana kwa pamoja kuunda Taasisi (Mamlaka) ya Muungano yenye wajibu wa kusimamia uvuvi wa eneo hilo la Uchumi la Bahari na pia Bahari Kuu kwa meli zenye kupeperusha Bendera ya Tanzania alisema Simbachawene.
Akihitimisha alisema kuwa, Uvuvi wa Bahari Kuu unatambulika Kimataifa kupitia Sheria ya Kimataifa ya Bahari ya mwaka 1982 hata katika mikutano mbalimbali ya kimataifa Tanzania huwakilishwa kama Nchi.