****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Jamii imetakiwa kuangalia njia zipi za kufuata ili kuwaepusha watu wenye msongo wa mawazo waachane na nia ya kutaka kujiua.
Ameyasema hayo msemaji wa jeshi la polisi,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa jeshi la polisi, SACP David Misime akitoa takwimu za miaka minne kwa watu waliojiua kuanzia mwezi Januari mpaka Juni.
Akizungumza na wanahabari SACP Misime amesema kuwa Watu wenye msongo wa mawazo wanatakiwa kuonana na wanasaikolojia na kuchunguzwa ili kuondokana na vitendo vya kutaka kujiua.
“Katika tafiti zetu za kukusanya hizi takwimu tumeona mara nyingi wanaojiua wengi hawaachi sababu za kujiua lakini wachache wanaacha sababu, wengine wanasema kwamba wamekataliwa na wapenzi wao, kuumwa kwa muda mrefu,maisha magumu pamoja na ugomvi wa kifamilia”.Amesema SACP Misime.
Aidha, SACP Misime amesema kuwa takwimu za miaka minne ya nyuma Januari hadi Juni kwa watu waliojiua zinaeleza kwamba, Waliojiua na sumu ni watu 75, waliojiua na kwa kujinyonga ni watu 367, Kujipiga risasi ni watu 5 huku waliojiua kwa kujichoma kisu ni watu 219.
Pamoja na hayo SACP Misime amesema kuwa wangetoa takwimu za mwaka mzima basi zingeongezeka kwa kiasi kikubwa.