Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George
Simbachawene akiwasilisha azimio la Itifaki ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur juu ya
uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na
matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa mbele ya Bunge hii leo mjini Dodoma. Ni itifaki
itakayosaidia juhudi za kuhifadhi mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa
kutambua madhara yanayoweza kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa
zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.
**********************
Bunge la Tanzania hii leo limeridhia Itifaki ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur juu ya
uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na
matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa.
Akiwasilisha azimio Bungeni Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) George Simbachawene amesema kuridhiwa kwa Itifaki
hiyo, Tanzania itaimarisha ushirikiano na Nchi Wanachama katika kusimamia na
kutekeleza masuala yanayohusu bidhaa au mazao ambayo yanatoka nje ya Nchi.
Aidha, imebainika kuwa Itifaki ya Nagoya – Kuala Lumpar itasaidia juhudi za
kuhifadhi mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara
yanayoweza kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa
mabadiliko ya kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.
Simbachawene amesema kuwa Itifaki hii itaongeza upatikanaji wa fursa za kujenga
uwezo wa wataalam nchini katika kusimamia matumizi salama ya bioteknolojia ya
kisasa na kusimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na
Kanuni za Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ya Mwaka
2009.
“Itifaki ya Nagoya – Kuala Lumpar itasaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira,
kulinda afya ya binadamu na wanyama dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya
bioteknolojia ya kisasa” alisisitiza Simbachawene.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kanali (Mst) Masoud Ali Khamis
ameishauri Serikali kuzipitia Sheria za nchi ambazo zitaenda sambamba na malengo
ya Itifaki kwa kuhakikisha nchi inanufaika.
Itifaki ya Ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu uwajibikaji kisheria na fidia kwa
madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa
ilianzishwa ili kuwezesha utekelezaji wa Itifaki ya Cartagena inayohusu Matumizi
Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ilipitishwa na Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Hifadhi ya Bioanuai Mwaka 2000 ambapo Tanzania iliridhia Itifaki hii mwaka 2003.