NJOMBE
Halmashauri ya mji wa Njombe ipo mbioni kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji bomba, baada ya serikali kukamilisha usanifu wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika mto hagafilo wenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita mil 17 kwa siku.
Kwasasa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Njombe NJUWASA imekiri kuwa na uwezo mdogo ambapo inatajwa kuzalisha lita mil 3 pekee kwa siku, wakati mahitaji ya mji yakiwa ni lita mil 12 jambo ambalo limeilazimu mamlaka hiyo kufanya mgao wa huduma hiyo ili kila mtaa uweze kuipata keki ya taifa.
Akizungumzia jitihada zinachukuliwa na serikali ili kumaliza changamoto hiyo mkurugenzi wa NJUWASA mhandisi John Mtyauli amesema kipindi kifupi kijacho wakazi wa mji wa Njombe watasahau adha ya mgao wa huduma hiyo kwani tayari serikali kupitia wizara ya maji imeshakamilisha usanifu katika mto Hagafilo ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita mil 17 kwa siku na kumaliza changamoto ya mgao.
Kuhusu suala la kuongezwa kwa tozo za maji Mhandisi Mtyauli amesema mamlaka zimelazimika kuongeza kiwango cha tozo kwa watumia maji ili kuisaidia mamlaka kupata fedha ili kuisaidia mamlaka hiyo kupata fedha kwa ajili ya kulipa mishahara watumishi wa umma, kuboresha miundombinu ya mifumo ya maji pamoja na mahitaji mengine ya mamlaka .
Amesema wizara iliyokuwa na dhamana ya kugharamia mambo yote muhimu katika mamlaka za maji kote chini imejitoa kwenye jukumu hilo hatua ambayo imezifanya mamlaka kuja na bei mpya ambazo kiini chake ni mapendekezo ya wananchi kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kujiendesha.
Katika hatua nyingine Wakati serikali ikifanya jitihada hizo za kuboresha huduma ya maji katika wa Njombe ambao unatajwa kukua kwa kasi zaidi kiidadi ya watu na kibiashara lakini wakazi wa mji huo wanasema wameziona jitihada hizo lakini bado kuna dosari katika utoaji wa huduma ya maji kwakuwa licha ya maji kutoka siku tatu au nne pekee katika wiki lakini bado tozo zake zimeonekana kuwa juu .
Kufuatia tozo hizo wanaiomba serikali kupunguza kidogo bei mpya zilizotangazwa ili kuwafanya wananchi kuwa na uwezo wa kulipa na kuendelea kufurahia huduma ya maji .
Awali tozo za maji ilikuwa ni shilingi 900 kiwango cha chini huku cha juu kikiwa ni 1100 , wakati bei mpya kiwango cha chini kikiwa shiling elfu 1449 huku cha juu kikiwa 1632.