**********************
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka
viongozi wa vyama vya Michezo nchini kuimarisha utawala bora ili kuwavutia
wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo na kuifanya michezo kuendelea.
Rai hiyo ameitoa leo tarehe 9 Septemba, 2019 wakati akiwaaga na kuwakabidhi
bendera wachezaji wa mchezo wa vishale nchini kuelekea katika mashindano ya wazi
ya nchi za Afrika Mashariki yatakayohusisha nchi nne ikiwemo mwenyeji Uganda,
Kenya, Tanzania na Rwanda, mashindano yanayotarajiwa kufanyika kwa siku tatu (3)
kuanzia tarehe 13 na kuhitishwa Septemba 15.
Aliendelea kuwa, utawala bora katika michezo unahusisha chama cha mchezo husika
kuwa na Ofisi, akaunti ya benki, mashindano ya ndani yatakayopelekea kupata timu
ya Taifa na wachezaji wenye viwango vya kiiwakilisha nchi katika mashindano ya
kimataifa pamoja na kuwa mipango mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuendeleza
mchezo.
“Kila wakati BMT na mimi binafsi nawasisitiza viongozi wa vyama vya michezo
kuimarisha Utawala bora ikiwemo kuwa na Ofisi, akaunti ya kuweka pesa za chama ili
kufanya maendeleo ya michezo husika, mipango ya muda mfupi na mrefu pamoja na
kuwa na mashindano ya ndani yatakayosaidia kupata wachezaji wenye viwango
wakuiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,”alisema na kuongeza
kuwa “Mkifanya haya yote mtawavutia wawekezaji kuwekeza katika michezo nchini na
kuifanya michezo iendelee,” alisisitiza Kaimu Mtendaji wa BMT Neema Msitha.
Kwa upande wake Nahodha wa timu ya Taifa ya mchezo wa vishale Noah Isaaya
ameeleza kuwa wachezaji wamejiandaa vizuri na wanaahidi kuutetea ubingwa wao,
ambapo amesema kuwa Tanzania itawakilishwa na wachezaji zaidi ya thelethini (30)
kutoka mikoa tofauti na mashindano hayo yatahusisha timu za taifa, vilabu, mchezaji
mmoja mmoja na wachezaji wawili wawili.
Wachezaji wa Tanzania katika mchezo wa vishale wanatarajiwa kusafiri kesho tarehe
10 Septemba, 2019 kuelekea nchini Uganda katika mashindano ya mchezo huo ya nchi
za Afrika ya Mashariki yanayotarajiwa kuanza kuanzia tarehe 13 na kumalizika
Septemba 15,2019.